Viongozi 7 wa madaktari waachiliwa huru

Angazo
Typography

Agizo hilo limetolewa na mahakama ya Rufaa Jijini Nairobi mapema leo.

Viongozi hao saba walifungwa Jumatatu baada ya kupatikana na hatia ya kutofuata uamuzi wa mahakama wa kumaliza mgomo wa madaktari ambao umedumu kwa miezi miwili unusu sasa.

Viongozi hao wametakiwa kuhakikisha suluhu ya mgomo huo inapatikana katika kipindi cha siku saba.

Mazungumzo ya kutafuta suluhu yataongozwa na Chama cha Wanasheria nchini (LSK) na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNHCR).

Madaktari wamekuwa wakiitaka serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara na kuboresha mazingira ya utendaji kazi hospitalini

Wanataka pia serikali iwekeze zaidi katika dawa, vifaa na mitambo hospitalini pamoja na kutoa pesa zaidi za kufadhili utafiti wa kimatibabu.

Wamekataa mshahara walioongezewa na serikali wa asilimia 40 wakisema kuwa ni wa chini kuliko ule walioafikiana mwaka 2013.

Karibu madaktari na wauguzi 5,000 kutoka hospitali 2,000 za umma, walianza mgomo wiki ya kwanza ya mwezi Desemba mwaka jana na wagonjwa wamekuwa wakikosa matibabu.