Wanyama pori wawahangaisha wakaazi wa Mkunumbi

Angazo
Typography

 

Akiongea na meza yetu ya angazo chifu wa kijiji hicho Mohammed Ali amesema ukosefu wa maji porini ndio sababu kuu inayopelekea wanyama hao kuingia mijini ili kutafuta maji ya kunywa.

Kulingana na chifu Ali mtu mmoja ameweza kuuwawa huku wengine saba wakijeruhiwa vibaya katika kijiji hicho tangu visa vya uvamizi wa wanyama pori kushuhudiwa.

Hata hivyo chifu Ali amesema serikali kupitia shirika la wanyama pori nchini KWS imeanza mikakati ya kutatua tatizo hilo linalowahangaisha wengi.

Amewashauri wakaazi wa kijiji hicho kutotoka nje usiku na wanafunzi wasiende shule mapema sana na kuwa waangalifu zaidi ili kujiepusha na hatari ya wanyama hao.

Wakazi wa kijiji hicho sasa wanaiomba serikali kufanya kila iwezalo ili kukabilaina na tatizo hilo.

Visa vya wanyama pori kuingia mijini vimekithiri sana katika kaunti ya Lamu tangu hali ya ukame ishuhudiwe kote nchini huku kisa cha hivi karibuni kikiwa ni kile cha hapo jana usiku  ambapo nyati zaidi ya 100 waliweza kuingia katika kijiji cha Mkunumbi kabla ya askari wa wanyama pori kuwadhibiti wanyama hao na kuwaregesha porini.