TUME YA NCIC YAAHIDI KIUFANYA KILA JUHUDI KUHAKIKISHA AMANI NA UWIANO UNADUMISHWA WAKATI WA UCHAGUZI MKUU WA AGOSTI 8.

Angazo
Typography

Akizungumza wakati wa kikao na wanahabari mjini Lamu Naibu Mwenyekiti wa NCIC Irene Wanyoike, amesema tume hiyo imeshirikiana na wadau mbalimnbali, ikiwemo ofisi ya Inspekta Mkuu wa Polisi, Joseph Boinnet, Wizara ya Usalama wa Ndani, kamati zote za usalama zikiongozwa na makamishna wa kaunti zote 47, Idara ya Mahakama (JSC ), Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali katika kufaulisha uchaguzi mkuu ujao.

Aidha Wanyoike amesema tume hiyo tayari imewapa maafisa wa usalama kote nchini mafunzo maalum yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza wakati wa uchaguzi.

Vile vile amedokeza kuwa zaidi ua maafisa 200 wamesambazwa kote nchini wakiwa na vifaa vya kunasa sauti na kamera za siri ili kukabiliana na yeyote anayetoa matamshi ya chuki wakati huu wa kampeni.

Kwa upande wake, Adan Abdi Mohammed, ambaye ni mmoja wa makamishna wa NCIC, waliozuru kaunti ya Lamu amewataka vijana kuepuka kutumiwa vibaya na wanasiasa ili kuzua fujo wakati huu ambapo kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 8 zinazidi kupamba moto.

Naye Profesa Gitile Naituli, amewapongeza wakazi wa Lamu kwa kudumisha amani na utulivu licha ya eneo hilo kushuhudia uvamizi wa magaidi uliopelekea watu zaidi ya 100 kufariki na mali ya mamilioni ya fedha kuharibiwa kati ya 2014 na 2015.

Tume hiyo imeanda msururu wa mkutano ya uwiano na amani kwa wadau mbali mbali katika kaunti ya Lamu wiki hii.