Wauguzi wa kaunti ya Lamu walalamikia kutishwa na barua za kinidhamu na serikali ya kaunti ya Lamu.

Angazo
Typography

Lakini wauguzi hao wamesisitiza kamwe hawatarudi kazini hata wakitishiwa kufutwa kazi hadi serikali kuu itakapokubali kutia sahihi mkataba wa makubaliano wa pamoja.

Kaimu katibu mtendaji wa kitaifa wa muungano wa wauguzi nchini (KNUN) Damon Kwaara akizungumza mjini Lamu amewataka wauguzi kote nchini wasikubali kupewa barua na serikali za kaunti na kuendelea na mgomo hadi bodi ya kitaifa ya muungano huo itakapotoa mwelekeo mwafaka.

Naye katibu mkuu wa muungano huo tawi la Lamu Julius Njogu amesema hawatakubali kutishiwa na barua za kinidhamu na kusisitiza kuwa ni haki yao kikatiba kushiriki mgomo.

Kwa upande wake Waziri wa afya katika kaunti ya Lamu Mohamed Kombo  amepinga madai ya wauguzi hao na kusema hakuna muuguzi yeyote aliyepewa barua ya kinidhamu.

Aidha Kombo amesema anasikitishwa na jinsi wauguzi wanavyoendeleza mgomo wao na kuwaomba kuwahurumia wagonjwa wanaoteseka hospitalini haswa wanawake wanaojifungua na kurudi kazini.

Mgomo huo wa wauguzi umeingia wiki ya tatu hii leo.