Aliyekuwa gavana wa Taita Taveta ajiunga rasmi na Jubilee

Angazo
Typography

Akizungumza baada ya kupokewa rasmi na rais Uhuru Kenyatta katika chama cha Jubilee katika uwanja wa Serani,  Mruttu amesema anaunga mkono kuchaguliwa tena kwa Kenyatta katika marudio ya uchaguzi wa urais ya Oktoba 26.

Mruttu amesisitiza kuwa atamfanyia kampeni rais Kenyatta katika kaunti ya Taita Taveta na Pwani ili kuhakikisha kuwa anashinda kinya’anyiro cha urais.

Amedokeza kuwa kuhamia chama cha Jubilee kumechangiwa na maendeleo mbalimbali yalioyotekelezwa na serikali ya chama hicho katika kaunti ya Taita Taveta na kote nchini kwa jumla.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya aliyekuwa seneta wa kaunti ya Mombasa na aliyewania ugavana kwa chama cha Wiper Hassan Omar Sarai kuuhama muungano wa NASA na kujiunga rasmi na chama cha Jubilee hapo jana.

Mruttu alichaguliwa gavana wa kwanza wa Taita Taveta mwaka 2013 kupitia chama cha ODM na baadae kuangushwa katika kura za mchujo wa chama hicho mwezi Aprili mwaka huu na aliyekuwa mbunge wa Wundayi Thomas Mwadeghu hali iliyomlazimu kuwania ugavana kwa mara pili kama mwaniaji huru na kuangushwa na Granton Samboja wa Wiper.