Familia ya Zinginzi yamtafuta mwanawao aliyetekwa nyara huko Likoni.

Angazo
Typography

Familia moja eneo la Likoni linaitaka serikali kuweka wazi aliko mwanawao anayedaiwa kutekwa nyara na watu wasiojulikana.

Kijana huyo kwa jina Mohammed Zingizi mwenye umri wa miaka 28,anadaiwa kutekwa nyara siku ya Ijumaa huko Likoni.

Munira  Zingizi,ambaye ni dada wa kijana huyo, amesema kuwa idara ya usalama imekuwa kimya juu ya swala hilo licha ya wao kupiga ripoti kwa vituo vyote vya polisi eneo la  Likoni.

Familia hiyo kwa sasa inataka idara ya polisi kuingila kati ili kujua endapo kijana huyo alikamatwa na polisi na pia waelezwe makosa aliyokamatiwa.

Nalo Shirika la kutetea haki za kibinadamu  la Haki Afrika limemtaka Inspekta mkuu wa polisi nchini Joseph Boinet  kuelezea hatua ambazo idara ya polisi imechukua kuhusiana na visa vya watu kupotea kwa njia tatanishi hususan hapa Pwani.

Mkurugenzi mkuu wa Haki Afrika Hussein Khalid, amesema takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 11 wamepotea kwa njia tatanishi kwa kipindi cha miezi mitatu sasa.

Huku hayo yakijiri baadhi ya wabunge kutoka  hapa  Pwani wamekemea vikali visa hivyo vya watu kupotea kiholela  wakisema kuwa lazima idara ya usalama iwajibike na kuwalinda wananchi.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa muungano wa wabunge wa Pwani ambaye pia ni mbunge wa Msambweni Suleiman Dori wamesema kuwa lazima waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiangi anafaa kuingilia kati na kuhakikisha kuwa visa hivyo vinasitishwa mara moja .Wabunge wengine ambao wamekuwa hapo ni yule wa Likoni Mishi Mboko, mbunge wa Mvita AbdulSwamad Sharifu Nassir na yule wa Kinango Benjamini Tayari.