25
Sun, Feb

Uhalali wa mbunge wa Changamwe kujulikana mwisho wa mwezi huu.

Angazo
Typography

Uhalali kuhusu ushindi wa mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi utajulikana mwishoni mwa mwezi huu katika mahakama kuu ya Mombasa.

Hii ni baada ya kesi ya kupinga ushindi wake kukamilika kusikilizwa leo mbele ya jaji Njoki Mwangi.

Jaji Mwangi amesema atatoa uamuzi wa kesi hiyo Februari 28 mwaka huu.

Kesi ya kupinga ushindi huo iliwasilishwa mahakamani na mgombea kiti cha ubunge kutipitia chama cha Jubilee Abdi Daib.

Wakili Gikandi Ngubwuin anayemwakilisha Daib ameitaka mahakama kufutilia mbali ushindi wa Omar Mwinyi kwa kusema kuwa ushindi wake sio wa halali.

Gikandi  ameutaja uchaguzi wa Agosti nane kuwa ulikumbwa na udanganyifu mwingi na wizi wa kura katika baadhi ya vituo vya kupigia kura eneo hilo la Changamwe.

Kwa upande wake wakili Mohammed Ali anayemwakilisha Omari Mwinyi ameutaja ushindi wa Mwinyi kuwa halali na akaitaka mahakama kutupilia mbali ombi la Daib.

Aidha, wakili huyo amemtaka Daib kulipa gharama ya shilingi milioni 15, huku wakili wa tume ya uchaguzi Justus Maithya akitaka kulipwa shilingi milioni kumi pindi uamuzi wa kesi hiyo utakapotolewa.

Kwa upande wake wakili wa Daib, ameipinga viwango hivyo vya fedha na kuitaka mahakama kuamua kiwango husika kinacho ambatana na gharama za kesi hiyo.