Kinyang`anyiro kikali cha Ugavana Mombasa na Kilifi

Siasa
Typography

Kufikia sasa hakuna mgombea yoyote aliyetangaza nia yake ya kuwani kiti hicho kupitia chama cha ODM anachowakilisha gavana Joho ingawa ushindani unatarajiwa kuwa kati ya vyama vya Wiper na Jubilee ambayo vyote viwili vina wagombea zaidi ya mmoja waliotangaza nia zao kuwania kiti hicho.

Seneta Hassan Omar aliye katibu mkuu wa Wiper atapimana nguvu katika mchujo na mbunge wa Nyali Hezron Awiti kutafuta tiketi ya chama hicho baada ya wote wawili kutangaza azma yao ya kuwania ugavana Mombasa.

Katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliondaliwa hapo jana uwanjani Tononoka, Awiti alimtaka kinara wa chama hicho Kalonzo Musyoka kutopendelea yeyote wakati wa kuamua ni nani atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika kuwania ugavana wa Mombasa.

Katika chama kipya cha Jubilee aliyekuwa mbunge wa Kisauni Anania Mwaboza vile vile ametangaza nia yake ya kuwania kiti hicho na anatarajiwa kupimana nguvu na mfanyibiashara Suleiman Shahbal.

Shahbal alishika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu uliopita kwa kura 94,905 wakati huo akiwa katika chama cha Wiper kinachounda muungano wa CORD huku gavana Joho, akishinda kwa kura 132,583.

Katika kaunti ya Kilifi gavana wa kaunti hiyo Amason Kingi amelazimika kuzungumza juu ya taarifa kwamba atafanya kazi na rais Uhuru Kenyatatta.

Katika kikao na waandishi habari Kingi amesisitiza kuwa ataendelea kubaki kwenye mrengo wa CORD huku akisema serikali ya jubilee imefeli katika kuwahudumia wakazi wa Kilifi.

Kingi anapokea upinzani mkali kutoka kwa mbunge wa Kilifi Kazkazini Gideon Mung`aro ambaye ni kinara wa Jubilee eneo la Pwani.

Mung`aro alitangaza azma yake ya kuwania kiti cha ugavana katika kaunti hiyo ya Kilifi hivyo kumenya na Kingi ambaye ni mmoja wa vigogo wa ODM hapa pwani.