25
Sun, Feb

Huduma za shirika la ndege la KQ zarudi rasmi baada ya kukatizwa

Uchumi/Biashara
Typography

Shirika hilo limesema abiria wote wamepewa mwongozo na kutoka sasa hakuna safari ya ndege itakayofutiliwa mbali baada ya kuimarisha utendakazi wao.

Mapema siku ya Jumapili shirika hilo lilikatiza usafiri wa ndege zake katika miji mbali mbali ulimwenguni na kuchlewesha baadhi ya safari hii leo baada ya wafanyakazi kususia kazi.

Wasimamizi walieleza kwamba tatizo hilo limetokea baada ya watu waliopewa mkataba kuingia kazini kutofika.

Taarifa hiyo imeeleza kwamba kutokana na sheria inayohitaji kiasi fulani cha wafanyakazi kuwa ndani ya ndege wameshindwa kulitimiza hilo kutokana na uhaba wa wafanyakazi na hivyo kufanya uamuzi mgumu wa kuzifuta safari nyengine.

Shirika hilo lilifuta safari za ndege zilizokuwa zije Mombasa, Sudan Kusini, Tanzania na Zimbambwe.

Shirika hilo limelazimika kuwalipia abiria wao ndege nyingine huku wakisema wanajutia jambo hilo.

Hili linajiri wakati shirika hilo linakabiliwa na hatari nyengine ya kupoteza mamilioni ya fedha kutokana na mgomo wa marubani wao utakaoanza Jumanne wiki hii.

Muungano wa marubani nchini (KALPA) umesema utafanya mgomo licha ya mahakama kuwazuilia ikisema marubani hawana mamlaka yoyote juu ya uongozi wa shirika hilo.

Shirika hilo katika miaka ya hivi karibuni limekuwa na mikosi mingi hadi kuathirika kwa faida yake.

Licha ya serikali kujaribu kulinusuru shirika hilo bado linayumbayumba.

Msemaji wa ikulu Manoeh Esipisu amesema swala hilo haliwezi kuzungumzwa katika mikao ya wanahabari kwa sababu KQ ni shirika lililoorodheshwa katika soko la hisa.