25
Sun, Feb

Matiangi: Visa vya wizi wa mtihani vyapungua mwaka huu

Habari Zaidi
Typography

Akizungumza katika shule ya msingi ya Jomo Kenyatta huko Msambweni, Matiangi amesema kwamba sheria mpya zilizoweka za kudhibiti wizi wa mitihani ya kitaifa zimefaulu pakubwa kwani zimepunguza kabisa visa vya udanganyifu  katika mtihani huo uliokamilika hii leo.

Amesema kwamba Sheria hiyo mpya  ya mitihani ya  kitaifa  inatarajiwa pia kutumika katika mtihani  wa kidato cha nne ikiwa ni katika jitihada za kukabili visa vya udanganyifu katika mitihani ya kitaifa.

Asema kwamba  serikali itaongeza idadi ya makasha ya  kuhifadhia makaratasi  ya mitihani ya kidato cha nne  KCSE ili kuhakikisha visa vya udanganyifu  havishuhudiwi tena huku akitoa onyo kali  kwa madalali ambao huwalaghai wanafunzi kwa kuwauzia   makaratasi bandia ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane  KCPE  pamoja na  ule  wa kidato cha nne  KCSE.

Matiangi aidha ameunga mkono hatua ya mratibu wa serikali ukanda wa pwani Nelson Marwa ya kupigwa marufuku usambazaji wa chakula kwa wanafunzi wanaokalia mtihani wa kitaifa akisema kwamba hatua hiyo pia ni miongoni mwa hatua za kuzuia udanganyifu.

Amesema kwamba wizara ya elimu haitaruhusu shughuli kama hizo zinazofadhiliwa na wanasiasa na kusema kwamba iwapo wanaolenga kuendeleza ugavi huo wa chakula sharti wapate ruhusu kutoka kwa mkurugenzi wa elimu wa kaunti husika.