25
Sun, Feb

Gambia inajiunga upya katika jumuiya ya madola.

Kimataifa
Typography

Takriban miaka mitano baada ya kujitoa katika jumuiya ya madola leo Gambia inajiunga upya.

Sherehe inafanyika leo katika makao makuu ya jumuiya hiyo mjini London kuidhinisha kurudi kwa nchi hiyo kama taifa mwanachama wa jumuiya ya madola.

Mnamo Februari 2017, rais mpya aliyechaguliwa Adama Barrow aliomba nafasi ya taifa lake kurudi kuwa mwanachama, na mwezi Desemba bunge nchini humo liliidhinisha ombi hilo la kurudi katika kundi hilo linalojumuisha mataifa yaliokuwa chini ya ukoloni wa Uingereza.

Gambia ilijiondoa katika jumuiya hiyo mnamo Octoba 2013.

Rais wa zamani Yahya Jammeh aliishutumu jumuiya hiyo kwa kile  anachokitaja "taasisi ya ukoloni mambo leo".

Aliishutumu Uingereza kwa kuwaunga mkono wapinzani wake wa kisiasa.

Yahya Jammeh alilitawala taifa hilo dogo la Afrika magharibi kwa miaka 22.

Alishindwa katika uchaguzi mkuu mnamo Desemba 2016 lakini akajaribu kufuta matokeo ya uchaguzi huo.

Ilichukua wiki kadhaa za majadiliano na tishio la jeshi kuingilia kati kumlazimisha aachilie madaraka.

Baada ya Afrika kusini, Pakistan na Fiji, sasa Gambia inakuwa nchi ya nne kurudi katika jumuiya ya madola.

KWA HISANI YA BBC SWAHILI.