25
Sun, Feb

Wanamgambo wawili wa IS raia wa Uingereza wazuiliwa Syria.

Kimataifa
Typography

Wapiganaji wa kikurdi nchini Syria wamewakamata wanamgambo wawili wa Uingereza wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu - IS wanaojulikana kwa jukumu lao katika mateso na mauaji ya mateka wa nchi za magharibi. 

Maafisa wa Marekani wamesema wapiganaji hao wawili wametambuliwa kuwa Alexanda Kotey na El Shafee Elsheikh. 

Walikuwa wanachama wawili wa mwisho wa kikundi kinachojiita Beatles cha wanamgambo wanne wa Uingereza waliokuwa mafichoni. 

Kiongozi wao alijulikana kama Mohammed Emwazi, raia wa Uingereza mwenye asili ya Kiarabu. 

Jihadi John, kama alivyofahamika, alionekana akiwauwa mateka, wakiwemo wanahabari wa Marekani Steven Sotloff na James Foley, katika video kadhaa za IS zilizoonesha watu wakikatwa vichwa. 

Aliuawa katika mashambulizi ya mwaka wa 2015 nchini Syria. 

Habari za kukamatwa Kotey na Elsheikh ziliripotiwa kwanza na gazeti la New York Times, ambalo lilisema watu hao wawili wanazuiliwa na wanajeshi wa Kikurdi nchini Syria wanaoungwa mkono na Marekani katika ngome za mwisho za wanamgambo wa IS nchini Syria kwenye Mto wa Euphrates kusini mwa mpaka na Iraq.

KWA HISANI YA DW SWAHILI.