25
Sun, Feb

UNHCR yasema wahamiaji wanyanyaswa kingono Ugiriki

Kimataifa
Typography

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuwahudumia Wakimbizi - UNHCR limesema limeorodhesha matukio kutoka kwa wanawake 180 katika mwaka wa 2017 ambao waliripoti kunyanyaswa kingono na kijinsia baada ya kuwasili Ugiriki. 

UNHCR imesema wahamiaji wako katika hatari ya kunyanyaswa kingono katika kambi ya Moria iliyoko visiwa vya Lesbos na kambi ya Vathy kwenye visiwa vya Samos. 

Msemaji wa shirika hilo Cecile Pouilly amewaambia wanahabari kuwa idadi kamili ya matukio ya unyanyasaji wa kingono inawezekana kuwa kubwa kwa sababu waathiriwa wengi wanaogopa kuripoti matukio hayo. 

Ameiomba serikali ya Ugiriki kuchukua hatua za kuwalinda wanawake na watoto katika kambi hizo za wakimbizi kwa kuwatengea maeneo maalum. 

Mashirika ya misaada mara kwa mara yameelezea wasiwasi kuhusu mazingira duni ya kuishi katika kambi za wakimbizi za kisiwa cha Aegean, ambako maelfu ya watu wanaishi wakati maombi yao ya hifadhi yakishughulikiwa.

KWA HISANI YA DW SWAHILI.