Wanawake eneo la Mwakirunge eneo bunge la Kisauni wanaelezea changamoto za ukosefu wa vyumba vya upasuaji maarufu kama Thieta katika Hospitali eneo hilo.

Kulingana na Phedis Mbura ambaye ni mwakilishi Wadi eneo hilo ni kuwa ukusefu wa vyumba hivyo kumepelekea wanawake wengi wajawazito wenye kuhitaji upasuaji kulazimika kusafiri kwenda katika hospitali kubwa ikiwemo hospitali kuu ya ukanda wa pwani kwa huduma hio.

Mbura ameeleza kuwa hali hio imesababisha wanawake kwa watoto kupoteza uhai wao huku akimuomba mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir kuliangazia suala hilo.

Akizungumza katika hafla iliyowaleta pamoja wakaazi wa eneo la Mwakirunge mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir amesema tayari ashapanga mikakati ili kuona kuwa tatizo hilo linalowakumba linapata suluhu.

Nassir ambaye anagombea kiti cha ugavana kaunti ya Mombasa amesema katika manifesto yake ya kwanza katika serikali ya kaunti moja wapo ni kupitisha bajeti ya pesa za kutosha na kuwahakikishia wakaazi huduma bora ya afya kwa wote huku akisisitiza haja ya kadi ya Bima ya afya ya NHIF kwa wazee wasiojiweza.