Jumla ya wanawake na vijana 2,500 kutoka vitongoji duni katika gatuzi dogo la Jomvu kaunti ya Mombasa wanatarajiwa kunufaika mafunzo tofauti ya mbinu tofauti za kujikimu kimaisha.

 Mradi huo umefadhiliwa na waqfu wa Coca-cola na unatekelezwa kupitia ushirikiano na shirika la kijamii la Shinning Hope For Communities (SHOFCO).

 Afisa mkuu wa kiufundi katika kampuni ya Coastal Bottlers Jane Gichanga amesema kuwa mradi huo ulianzishwa ili kuhakikisha kuwa wanawake pamoja na vijana wanapata mafunzo na ujuzi kabla ya kupewa pesa za kujianzishia miradi mbalimbali itakayowawezesha kujikimu kimaisha.

Akizungumza akiwa huko Bangladesh wakati wa kuzindua mradi huo, Gichanga amesema jumla ya shilingi milioni 28 zilitengwa kuufanikisha mradi huo ikiwemo kwa mafunzo na mikopo kwa walengwa na ulianzishwa Septemba mwaka wa 2021 na unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu akiwataka wale watakaopewa mikopo hiyo kuitumia kujifanikisha kimaisha.

Kauli yake imeungwa mkono na afisa wa miradi katika shirika la SHOFCO Gladys Mwende akiongeza kuwa mradi huo wa mwaka mmoja umeweza vilevile kuwafaidi wanawake na vijana sehemu tofauti za nchi na kwamba wao hufuatilia na kuwapa mafunzo zaidi ya namna ya kujikuza na kuendeleza biashara zao.

 Kwa upande wake Nuru Mwanyoka mmoja miongoni mwa walengwa wa mradi huo akipongeza ujio wa mradi huwa kwamba unatawasaidia kujiimarisha kimaisha kwa kuinua biashara zao.

 Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo