Umoja wa Mataifa umesema utaanzisha uchunguzi wa mashambulizi dhidi ya gereza moja mashariki mwa Ukraine linaloshikiliwa na Urusi.

Jeshi la Urusi lilisema wafungwa 50 wa kivita waliuawa na wengine 73 kujeruhiwa katika mashambulizi ya wiki iliyopita dhidi ya gereza la Olenivka.

Kyiv na Moscow zinashutumiana kwa mashambulizi hayo katika eneo la Donestk.Urusi inasema Ukraine ilifanya mashambulizi hayo kuwazuwia wanajeshi wake kujisalimisha kutokana na kuishiwa na matumaini.

Ukraine inaituhumu Urusi kulishambulia gereza hilo ili kuficha mateso na mauaji yake kwa wafungwa wa kivita wa Ukraine.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesema mataifa yote mawili yameomba uchunguzi ufanyike.Ameongeza kuwa hadidu rejea za uchunguzi huo, ambazo zitahitajika kukubalika na pande zote mbili, zinatayarishwa.