Wanafunzi wakiwa na magunia ya chupa za plastiki

Utunzaji wa mazingira umekua changamoto kubwa sana kote ulimwenguni kwani mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri vigezo vingi katika jamii ikiwemo afya, hewa safi, maji safi ya kunywa, chakula na makazi salama.

Fatuma Hamisi mwenye umri wa miaka 13 ni mwanafunzi katika shule ya msingi ya Salex Transition Academy iliyoko eneo la Mtongwe kaunti ya Mombasa. Yeye ni mwanafunzi wa gredi ya 6 na pia ni miongoni mwa wanafunzi wanaojishughulisha na utunzaji wa mazingira katika shule hiyo.

Fatuma na wenzake hupeana chupa za plastiki na kisha kupewa miche ya miti sodo na vitabu kama njia moja wapo ya kukabili mabadiliko ya tabia nchi.

Kulingana na national geographic - Nat Geo, Kila mwaka, takriban tani milioni 8 za taka za plastiki hurushwa baharini kutoka mataifa ya Pwani.

Kila siku Fatuma anahakikisha shule yao haina chupa za plastiki zilizotapaka ovyo. Yeye huziokota chupa hizo na kuzikabidhi kikundi cha kutunza mazingira cha Kishoka Youth ambao utumia chupa hizo katika kutengeneza bidha mbali mbali kama vile viti, meza, vipuli na hata kujenga nyumba kutumia chupa hizo.

Fatuma na wenzake katika shule hiyo hupokea vitabu, kalamu,miche ya miti na hata sodo huku na wao wakipeana chupa za plastiki walizoziokota kwa kikundi cha Kishoka Youth. Hatua hii inasaidia kuwapa motisha wanafunzi wenzake katika kujizatiti kwa utunzaji wa mazingira.

Geofrey Anari ambaye ni mwanafunzi wa darasa la nane anaema mwanzoni wazazi wake walimshanga na hata kumkataza walipomuona akiokota chupa za plastiki, ila alipowaelezea manufaa ya kuokota chupa hizo, wazazi wake walimuelewa na kumuunga mkono kwani wao pia wanamsaidia katika kuokota chupa za plastiki.

“Wazazi wangu waliponiona naokota chupa za plastiki, waliona kama mzaha na kuanza kunicheka, ila nilipowaelimisha kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira, basi walinielewa na kuniunga mkono na wao pia wanaokota chupa na kuniwekea,”Geofrey anasema.

Kufikia sasa wanafunzi wa shule hiyo wamepanda zaidi ya miche 30 waliyopewa na kikundi cha Kishoka Youth kama njia moja wapo ya kuwahusisha wanafunzi katika utunzaji wa mazingira.

“Tumeapanda miti zaidi ya 30 ambayo tulipewa na Kishoka Youth na sisi tukawapa chupa za plastiki, bado tutaendelea kushirikiana katika kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo,”Alisema Geofrey.

Hamisi Mohammed, ambaye ni msemaji wa kikundi cha kulinda mazingira cha Kishoka Youth, alisema kuwa mwaka huu wamegawa miti zaidi ya 100 kwa wanafunzi.Anasema kwa sasa wanakabiliwa na ukosefu wa fedha ndiposa hawajatoa miti mingi ikilinganishwa na mwaka jana.

Hamisi, anafafanua kwamba waliamua kuwashirikisha wanafunzi katika utunzaji wa mazingira ili wawe na ufahamu na kusaidia jamii, ikizingatiwa watoto wengi hawana ufahamu wa kutunza mazingira.

“Wanafunzi ama watoto ndio wanafaa katika kutunza mazingira kwa sababu ni rahisi wao kuelewa kwa haraka na pia wanaweza kuelimisha wazazi wao nyumbani. Kwa sasa wanafunzi wengi hawana ufahamu wa kutunza mazingira ndiposa tukaamua kuwashirikisha,”anasema Hamisi.

Kauli ya kuhusisha wanafunzi katika utunzaji wa mazingira imepigiwa upatu na mkurugenzi mku wa shule ya Salex Transition Academy Felix Savai. Savai anasema katika shule hiyo wanazingatia sana kuelimisha wanafunzi namna ya kutunza maazingira na madhara ya kuharibu mazingira. Anasema wanahakikisha wanapanda miti na kuokota chupa za plastiki kama njia ya kuepuka uchafuzi wa mazingira.

Aliongeza kuwa tangu mradi huo uanzishwe katika shule hio, imesaidia sana kwani awali eneo hilo lilikuwa limejaa chupa za plastiki,ila kwa sasa sio rahisi kupata chupa eneo hilo kwani wanafunzi wamekuwa waangalifu.

 “Wanafunzi waliupokea kwa uzuri mradi huo, akitaja kuwa wanafunzi hukusanya chumpa nyingi na kuzikabidhi kikundi cha Kishoka. Aidha anataja kuwa mradi huo ulikuja wakati mwafaka kwani unawiana na mtaala mpya wa CBC”Anasema Felix.

Kwa upande wake, Hamisi anaelezea kuwa mwanzoni walipokuwa wakianza mradi wao, wanafunzi na jamii iliwacheka na kuwakejeli, ila baada ya kuwaonyesha bidhaa zinazotokana na chupa za plastiki, ndipo pale wakaanza kupata uungwaji mkono.

Mwanamisi Juma na Salim Mwinyi, ni wanajamii ambao wanaupongeza mradi huo wa kuhifadhi mazingira, wakisisitiza kuwa jamii imeanza kushirikiana na kikundi cha Kishoka Youth.

Mwanamisi alisema yeye binafsi uokota chupa za plastiki na kuzikabidhi kikundi hicho. Alisema chupa hizo pia hutengenezwa bidhaa kama meza. Alisisitiza kuwa tangu mradi huo uanzishwe mtaa wao umekuwa safi na sio rahisi kupata chupa zilizotupwa ovyo ovyo.

Hamisi anahimiza jamii kutumia chupa za plastiki katika kujengea nyumba zao badala ya kutumia mawe, kwani uchimbaji wa mawe pia unachangia uharibifu wa mazingira.

“Chupa za plastiki zimejaa kila mahali, ni bora tuzijenge nyumba badala ya kuziacha kuendelea kuharibu mazingira,tusitumie tena mawe kwani uchimbaji wa mawe pia ni uharibifu wa mazingira,”Alisema Hamisi.

Mwanafunzi Geofrey hakusita kutoa wito kwa wanafunzi wengine kutoka shule mbali mbali kukumbatia uokotaji wa chupa na kupanda miti kama njia ya kutunza mazingira kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

 

Sikiliza Sauti ya Makala haya yaliyopeperushwa redioni.

 Makala yamedhaminiwa na Jhr.Mwandishi:Rose Tawa.Muhariri:Athuman Luchi