Baraza la maimamu na wahubiri nchini Kenya CIPK limesema litashirikiana na washika dau mbali mbali ili kukabiliana na donda sugu la utumizi wa mihadarati.

Akizungumza na wanahabari hapa Mombasa katika ofisi za baraza hilo, katibu mkuu wa baraza hilo sheikh Mohammed Khalifa amesema kuwa vita dhidi ya mihadarati vinahitaji juhudi za pamoja.

Khalifa ametaka asasi za kiserikali kuendeleza vita dhidi ya mihadarati hadi katika dawa zengine za kulevya.

Aidha Khalifa amesema kwamba utumiaji wa dawa za kulevya umekua janga sugu nchini Kenya, huku akisema kuwa fedha nyingi zinatumika kila siku katika biashara hio.

Kwa upande wake sheikh Mohammed Dori ameshangazwa na hatua ya kupigwa marufuku kwa bhangi na kuhalalishwa kwa miraa huku akisema athari zote ni sawa.

 

Gavana wa kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir pamoja na wa Embu Cecil Mbarire wamekutana hapa Mombasa ili kujaribu kutatua mzozo uliopo kuhusu zao la miraa na Mugokaa.

Magavana hao wawili wamekubaliana kuunda timu ambayo itatengeza sheria zitakazotoa muongozo kuhusu biashara hio.

Katika mkutano huo, gavana Nassir amesema kuwa biashara hio imepelekea vijana wengi kuishia katika vituo vya kurekebisha tabia kutokana na ulaji wa miraa na mugokaa.

Aidha Nassir amesema kuwa hana uwezo wa kupiga marufuku bidhaa hizo kuingi katika kaunti ya Mombasa kutokana na sheria iliyopo kuhusiana na miraa na mugoka.

Kwa upande wake gavana wa kaunti ya Embu Cecil Mbarire ameisihi serikali ya kaunti ya Mombasa kuunda sheria zitakazodhibiti biashara hio.

 

Maafisa wa upelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, wamemkamata raia wa Nigeria kwa madai ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
Mshukiwa huyo anadaiwa kupatikana na gramu 200 za kokeini yenye thamani ya takriban shilingi 600,000.
DCI inasema kukamatwa kwa Victor Chinenye Ikonne kulifuatia oparesheni ya kijasusi ambapo polisi walivamia nyumba yake ya kukodisha iliyoko eneo la Utange-Kisauni, kaunti ya Mombasa.
Mshukiwa amepelekwa katika kituo cha polisi cha bandari akisubiri kufikishwa mahakamani.

Jamii ya mtaa wa old town imepongeza hatua ya gavana wa mombasa Abdulswammad Shariff Nassir kuongezea ushuru miraa na mugokaa.

Jamii hiyo imelaani utumizi wa miraa na mugoka hapa mombasa ikisema utumizi huo umechangia utovu wa usalama na wizi katika sehemu mbalimbali hapa Mombasa

Akiongea na wanahabari daktari Jalabi Ashraf amesema idadi kubwa ya talaka zimechangiwa na utumizi wa miraa na mugoka.

Ameeleza kwamba wazazi wanaotumia miraa na mugoka wamesahau majukumu yao ya kusomesha watoto wao kwa kuwa wanatumia pesa nyingi kwenye mihadarati huku akitoa wito kwa wazazi kuwa vielelezo bora kwa vizazi vyao ili kuepusha vizazi hivyo kuiga mienendo yao michafu.


Kwa upande wake imamu wa msikiti Huda Spaki Abu Hamza ameunga mkono agizo la gavana wa Mombasa la kupiga marufuku uuzaji wa miraa na mugoka karibu na taasisi za elimu.

Abu Hamza aidha amemtaka gavana kupiga marufuku uuzaji wa mugoka na miraa katika soko la kongowea akisema kuwa soko hilo linafaa kuwa la chakula peke yake.

 Wakati uo huo ametoa wito kwa magavana za kaunti za pwani kushirikiana katika suala hili ili kuokoa jamii ya pwani dhidi ya utumizi wa mihadarati.

 

Rais William Ruto ametangaza kuwa shule zote zitafunguliwa Jumatatu, Mei 13.
Tangazo hili llinajiri wiki moja baada ya serikali kuahirisha ufunguzi wa shule kwa muda usiojulikana.
Rais ameyasema hayo baada ya idara ya utabiri wa hali ya anga kusema mvua itaendelea kupungua.
Aidha rais amewataka wazazi kutokuwa na wasiwasi kuhusu mazingira ya shule za watoto wao kutokana na mvua.
Serikali imesema pesa za ukarabati wa shule na asasi nyenginezo za masomo zilizo athirika na mvua zitakarabatiwa kupitia hazina ya ustawishaji maeneobunge NG-CDF.

Show more post