Tume ya elimu ya chuo kikuu imebatilisha shahada ya chuo kikuu ya seneta wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja kutoka chuo kikuu cha Team nchini Uganda.

Katika barua iliyoandikwa na tume hiyo inasema imepokea malalamishi kuhusu uhalali wa shahada hiyo katika somo la Science in Management.

Tume hiyo imesema kuna uhitaji wa uchunguzi zaidi kufanywa kuhusiana na uhalali wa cheti hicho.Tume hiyo tarehe 6 mwezi huu ilimuandikia barua seneta huyo ikithibitisha kutambua cheti hicho.

Walalamishi wanne walikuwa wamewasilisha kesi mahakamani kupinga kuidhinishwa kwa Sakaja kuwania kiti hicho ,kwa madai ya kuwa na cheti ghushi cha chuo kikuu.

Chuo kikuu cha Nairobi kimetoa taarifa na kusema kuwa Sakaja angali anaendelea na masomo chuoni humo na walaa hajafuzu.

Ikumbukwe kuwa malalamishi hayo yameibuka tangu Sakaja aidhinishwe kuwania kiti cha ugavana kaunti ya Nairobi na tume ya IEBC tarehe 7 Juni.