Mbunge wa Kinango Gonzi Rai amewataka wakaazi wa eneo bunge la Kinango kutohofia kuhusu suala la Mswada wa kifedha wa mwaka 2023/24.

Kulingana na mbunge huyo, iwapo Mswada huo utapitishwa bungeni, wakaazi wa kinabgo watafaidika kwa asilimia kubwa kwa kuwa mswada huo umezingatia sana maswala ya ujenzi wa Barabara za eneo bunge miongoni mwa miradi mingine.

Amesema mswada huo utamuwezesha kutekeleza miradi mbalimbali ya kumfaidisha mkaazi wa kinango huku akitoa wito kwa wakaazi kujitenga na propaganda zinazoenezwa kuhusu mswada huo.

Haya yanajiri huku naibu rais Rigathi Gachagua akiwahimiza Wakenya waendelee kuvumilia wakijaribu kufufua uchumi.

Akitetea mswada wa Fedha 2023, Gachagua amesema ni sawa kwa serikali kufanya maamuzi magumu na yasiyopendeza kwa manufaa ya wananchi.

Gachagua amebainisha kuwa pindi tu Bunge la Kitaifa litakapopitisha Mswada huo, utasaidia serikali kupata pesa kufufua uchumi.

Ameeleza kuwa kwa sasa serikali ina deni la Sh9.6 trilioni hivyo basi ni lazima wakusanye ushuru wa kujenga barabara na kuendeleza miradi mingine.

Amesema kuwa utawala wa Kenya Kwanza unawawazia Wakenya mema na kwamba serikali inalenga kuboresha uchumi.