Jumuiya ya IGAD imetoa wito kwa mataifa ya bara Afrika kuwekeza zaidi katika uchumi samawati ili kuchangia katika mapato ya mataifa yao.

Katika taarifa yake iliyosomwa na mwakilishi wa IGAD humu nchini dkt Fatma Adan, katibu mkuu wa IGAD Dr Workneh Gebeyehu ameeleza kuwa sekta ya uchumi wa baharini ni muhimu kwa bara Afrika na huenda ikawa moja wapo ya sekta zitakazochangia kwa kiasi kikubwa mapato na ukuwaji wa uchumi.

Amedokeza kuwa sekta hiyo ni muhimu haswa wakati huu ambapo mataifa ya Afrika yanapoteza asimilia 15 ya mapato yake kutokana na mabadiliko ya hali ya anga.

Jumuiya hiyo imetoa wito wa kufanyiwa uvumbuzi zaidi sekta hiyo katika uimarishaji wa usafiri, kawi, chakula na bayoteknolojia ili kuwa na udhabiti wa maendeleo humu nchini.

Kwa upande wake gavana wa Lamu Issa Timamy ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya uchumi samawati katika baraza la magavana, ametoa wito kwa washikadau kuongeza juhudi za kuhakikisha mazingira ya baharini yanakuwa salama dhidi ya plastiki.

Timamy amekariri ripoti ya Umoja wa Mataifa inayoeleza kuwa zaidi ya tani milioni 8 za uchafu wa plastiki huelekezwa baharini na kwamba kufikia mwaka 2050 bahari zitakuwa na uchafu mwingi wa plastiki kuliko samaki.

Viongozi hao walikuwa wakizungumza hapa Mombasa katika kongamano la siku nne kwa lengo la kutafuta mwafaka wa kuendeleza uchumi samawati.