Idara ya afya kaunti ya Mombasa imewahimiza wazazi walio na watoto chini ya miaka mitano kuwapeleka watoto hao kupewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio ambao husababisha tatizo la kupooza kwa viungo vya mwili.

Afisa mkuu wa afya ya umma katika kaunti ya Mombasa daktari Salma Mohammed amesema chanjo hiyo inatolewa baada ya kugundulika kwa viini vya polio katika baadhi ya maeneo hapa Mombasa.

Amedokeza kuwa kati ya watoto 100, tisini kati yao wako katika hatari ya kuwa viini hivyo hatari na wanalenga takriban watoto  323, 620 wanaolengwa kupokea chanjo hiyo.

Shughuli ya chanjo hiyo itafanyika katika kaunti 13 za humu nchini Mombasa ikiwa moja wapo kuanzia tarehe 22 hadi 26 mwezi huu wa Mei na lengo lake ni kuwafanya watoto wadogo kuwa na kinga ya mwili ya kutosha.

Afisa wa kuhamasisha katika kaunti ya Mombasa Caroline Agutu amesema mbali na zoezi hilo kutekelezwa nyumba hadi nyumba, vituo vya afya vilevile vitatoa chanjo hiyo kwa walio karibu navyo.

Aidha amepuuza madai yanayosmbazwa kuhusiana na chanjo hiyo na kusema kuwa chanjo hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu akiwahimiza wananchi kutoingiza itikadi potofu.