Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho amehukumiwa kifungo cha siku 60 jela au faini ya shilingi 250,000 kwa kosa la kudharau amri ya mahakama.

Gavana Joho alishtakiwa pamoja na mwakilishi wadi wa Changamwe, Bernard Ogutu.

Kwa upande wake Ogutu ametozwa faini ya shilingi 20,000, au kutumikia kifungo cha siku 14 jela.

Jaji Munyao Sila, aliyetoa uamuzi huo ametoa hati ya kukamatwa kwa wawili hao, na kuamuru wapelekwe katika gereza la Shimo La Tewa hadi pale watakapotoa uthibitisho wa malipo ya dhamana.

Ashok Doshi, mfanyabiashara wa Mombasa, aliwasilisha kesi hiyo katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi mnamo 2019.

Madai yake yalikuwa kwamba anamiliki sehemu ya ardhi huko Changamwe, Mombasa, ambayo ilivamiwa na maafisa wa Kaunti ya Mombasa mnamo Februari 25, 2019, na kusababisha machafuko na uharibifu.

Doshi alikwenda mahakamani na kupata amri ya kuzuia maafisa wote wa Kaunti ya Mombasa, na wafanyikazi kufika kwenye ardhi yake.

Licha ya agizo la mahakama Joho na Ogutu, wakiambatana na mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi pamoja na vijana zaidi ya 100 walivamia ardhi hiyo mnamo Mei 10, 2019 na kusababisha machafuko na uharibifu zaidi.


 

More Stories

Buriani jenerali Francis Ogolla

Idara ya polisi yasema mgomo wa madaktari ni usumbufu

Seneta Miraj amtetea waziri wa afya

Bandari ya Lamu kuipiku ile ya Mombasa asema Mbogo