Wakili Miguna Miguna amesema hatavumilia tena kuwa raia wa Kenya iwapo kinara wa ODM Raila Odinga atanyakua kiti cha urais katika chaguzi kuu za mwezi Agosti.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Miguna amedai kwamba yuko tayari kuuza mali yake yote na kukana uraia wake wa Kenya iwapo aliyekuwa waziri mkuu atatwaa urais baadae mwaka huu.

Miguna ambaye amekuwa akiishi Canada tangu mwaka wa 2018 ambapo alifurushwa kutoka nchini anajulikana kuwa na uraia wa Kenya na Canada.

Wakili huyo alifurushwa kutoka nchini Kenya mnamo Machi 2018, miezi michache tu baada ya kumuapisha kinara wa ODM Raila Odinga kama rais.

Miguna amesisitiza kwamba angali anaamini Raila alishinda chaguzi za 2007 na 2017 na ndio maana akakubali kumuapisha.

Hivi majuzi Miguna amekuwa akimkosoa kinara wa ODM Raila Odinga pamoja na rais Uhuru Kenyatta huku akiwashtumu kwa kuzuia kurudi kwake.

Hata hivyo sasa amedai kuwa waziri huyo mkuu wa zamani hawezi kushinda uchaguzi wa mwaka huu kwa njia ya kuaminika.