Mgombea wa ugavana kaunti ya Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amesema atapambana na wabadhirifu wa pesa za umma endapo atachaguliwa kuwa gavana wa jimbo la Mombasa.

Akizungumza na wadau mbalimbali katika sekta ya Utalii katika ukumbi wa Whitesands eneo bunge la Nyali,Nassir ametaja suala la ubadhirifu wa fedha za umma kama miongoni mwa masuala humu nchini ambayo yanaregesha nyuma maendeleo.

Nassir ambaye anaazimia kumtithi gavana Ali Hassan Joho ameeleza haja ya kuzibwa kwa mianya inayotumiwa kufuja pesa za umma ili kuunda uongozi bora.

Kulingana naye asilimia 30 ya fedha katika serikali ya kaunti hupotea akisema mara nyingi hupotea mifukoni mwa watu binafsi.

Kwenye suala la utalii Nassir amesema ataangalia mswada wa usimamizi wa fuo za Bahari uliopendekezwa na wadau hao sawia na kuunda jopo kazi litakaloangazia masuala mbalimbali yanayoikumba sekta hiyo.

Akiangazia suala la afya Nassir amesema kuwa ananuia kuunda jopo kazi la afya,Jopo ambalo litakuwa ni lenye kutoa mapendekezo kwa serikali ya kaunti kuhusu huduma bora za afya kwa wananchi.