Zaidi ya familia 80 zilizoathirika na mradi wa ujenzi wa mtambo wa saruji katika eneo la Mwachome eneo bunge la matuga huko Kaunti ya Kwale zimeanza kupokea fidia ya ardhi zao.

Kulingana na mbunge wa Matuga Kassim Tandaza, familia hizo zinazoishi katika ardhi ya ekari 400 tayari zimeanza kufidiwa na kampuni ya saruji ya Bamburi.

Tandaza amedokeza kwamba waathiriwa wa mradi huo watapokea kati ya shilingi milioni 10 hadi 15 kupitia kamati za ardhi zilizoundwa katika eneo hilo.

Itakumbukwa kuwa mradi huo awali ulikuwa utekelezwe katika eneo la denyenye lakini kutokana na mzozo wa ardhi ukahamishwa eneo la Mwachome.

Kwa upande wa baadhi ya wakaazi katika eneo hilo wameipongeza kampuni hiyo kwa kuanzisha mpango wa kuwaelimisha kuhusu mradi huo.

Wakiongozwa na Khamis Mzungu wakaazi hao watakaolipwa fidia wameeleza kuwa elimu hiyo inalenga kuwasaidia katika utumizi wa fedha hizo.