Serikali ya kaunti ya Kwale imelitaka shirika la huduma kwa wanyamapori nchini (KWS) kutatua suala la mizozo ya binadamu na wanyamapori ambalo limekuwa donda sugu katika kaunti hiyo.

Kupitia naibu gavana wa kaunti hiyo Chirema Kombo amesema kuwa visa vya ndovu kuvamia mashamba na kuharibu mimea ya wenyeji vimeongezeka katika maeneo tofauti ambayo mara kwa mara huathirika na ukame.

Akizungumza na wanahabari, Kombo amelitaka shirika hilo kuingilia kati na kuwaondoa mara moja ndovu hao ambao wamekuwa tishio kubwa kwa usalama wa chakula kinachotegemewa na wenyeji.

Kauli hiyo imeungwa mkono na meneja wa shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Pwani Hassan Musa aliyetoa tahadhari kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa mapema, basi huenda wakaazi wa Kwale wakaathirika na baa la njaa.

Musa ameitaka KWS kuchukua hatua za haraka za kuwakabili ndovu hao baada ya wakaazi kaunti hiyo kupanda mimea yao msimu huu wa mvua.