Mizozo kati ya wafugaji na wakulima katika eneo la Hindi Lamu Magharibi imetajwa kupungua kwa kiwango kikubwa.

Mwenyekiti wa kamati ya wafugaji na wakulima eneo la Hindi Hassan Chonde amesema hii imechangiwa na kamati hiyo kufanya mazungumzo ya amani mara kwa mara baina ya wafugaji na wakulima wa eneo hilo.

Amesema awali kulikuwa hakuna mpango wowote wa kuleta jamiii hizo mbili pamoja hivyo basi mizozo ilikuwa ikishuhudiwa mara kwa mara baina yao.

Aidha amehimiza serikali ya kaunti ya Lamu kuharakisha mchakato wa kutengewa aridhi wafugaji kwa ajili ya malisho.

Amesema hii itakuwa njia mwafaka ya kudhibiti mifugo kuingia katika mashamba ya watu kwani wafugaji wamekuwa wengi na mifugo imeongezeka mara dufu.