Serikali ya kitaifa imeanza rasmi ziara ya siku mbili ya kukagua miradi ya serikali kuu katika ukanda wa Pwani.

Ukaguzi huo unasimamiwa na Kamati ya kitaifa ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya serikali ikiongozwa na mwenyekiti wake daktari Karanja Kibicho ambae pia katibu katika wizara ya usalama wa ndani.

Ziara hiyo imeanza rasmi kwenye Bandari ya Mombasa, ambapo Kibicho amekagua ujenzi wa eneo jipya la kuegesha makasha pamoja na ujenzi wa kituo cha pakua mafuta ya ghafi kutoka kwa mataifa ya nje.

Katibu huyo aidha amesema kuwa lengo la kuzuru Bandari ya Mombasa ni kuona kuwa miradi hiyo imetekelezwa ipasavyo ili kuboresha utendakazi wa Bandari hiyo.

Wakati uo huo, Kibicho amedokeza kuwa kamati hiyo iliundwa na rais Uhuru Kenyatta ili kusimamia utekelezaji mwafaka wa miradi inayozinduliwa na serikali kote nchini na kwamba imegawanywa katika makundi manne ikiongozwa naye kama mwenyekiti.

 Mwandishi:Ibrahim Mudibo