Maafisa wawili wa polisi wamejiuwa kwa kujipiga risasi katika visa tofauti katika Kaunti ya Mombasa usiku wa kuamkia Jumanne.

Kulingana na taarifa kutoka kwa Wakuu wa usalama Kaunti ya Mombasa Afisa wa GSU Dennis Kamau amepatikana nyumbani kwake huko Nyali akiwa amefariki mapema siku ya Jumanne.

Afisa huyo alikuwa katika kikosi maalum kinachotoa ulinzi kwa Maafisa wa ngazi za juu Serikalini na anadaiwa kujipiga risasi kichwani kwa bastola na kufariki papo hapo.

Katika tukio la pili, Afisa wa polisi David Koech anayehudumu katika kituo cha polisi cha Concordia huko Kiembeni Kaunti ya Mombasa amejipiga risasi kifuani na kujiuwa papo hapo katika tukio la kutatanisha.

Polisi wamepata bunduki aina ya AK-47 na jumla ya risasi 29 kwenye kasha la risasi ya bunduki hiyo.

Uchunguzi tayari umeidhinishwa huku miili hiyo miwili ikipelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali kuu ya rufaa kanda ya Pwani.

Mwandishi:Ibrahim Juma Mudibo