Ghana imethibitisha visa vyake viwili vya kwanza vya virusi hatari vya Marburg, ugonjwa unaoambukiza sana katika familia moja na virusi vinavyosababisha Ebola.

Inasema wagonjwa wote wawili walifariki hivi majuzi hospitalini katika eneo la kusini mwa Ashanti.

Maafisa wa afya katika taifa hilo la Afrika Magharibi wanasema watu 98 sasa wako chini ya karantini.

Bado hakuna matibabu kwa Marburg - lakini madaktari wanasema kunywa maji mengi na kutibu dalili maalum kunaboresha kinga.

Virusi hupitishwa kwa watu kutoka kwa popo wa matunda na huenea kati ya wanadamu kupitia upitishaji wa maji ya mwili.

Ni ugonjwa mbaya, ambao mara nyingi husababisha kifo na dalili kama vile maumivu ya kichwa, homa, maumivu ya misuli, kutapika damu na kutokwa na damu.

Maafisa wanaonya watu kujiepusha na mapango na kupika vizuri bidhaa zote za nyama kabla ya kula.

Barani Afrika, milipuko ya awali na visa vya mara kwa mara vimeripotiwa katika Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Afrika Kusini na Uganda, WHO inasema.

Mlipuko wa kwanza kabisa wa Marburg ulikuwa nchini Ujerumani mnamo 1967 ambapo watu saba walikufa.

Virusi hivyo viliua zaidi ya watu 200 nchini Angola mwaka 2005, mlipuko mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa kulingana na shirika la afya duniani.


 

More Stories

Buriani jenerali Francis Ogolla

Idara ya polisi yasema mgomo wa madaktari ni usumbufu

Seneta Miraj amtetea waziri wa afya

Bandari ya Lamu kuipiku ile ya Mombasa asema Mbogo