Hali ya ukame iliyosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi imepoteza rasilimali, na kuua mifugo ambayo ni tegemeo la jamii za wakazi wa Kinango,Samburu na Lunga Lunga kaunti ya Kwale.Kiangazi hicho kimeziacha familia nyingi maeneo hayo kwenye lindi la umaskini.

Ufukara na Mabadiliko hayo ya tabia nchi imewafanya mabinti kutoka kwa Familia nyingi zilizoathirika kuacha shule na kukimbilia ndoa za mapema,huku wengine wakipachikwa mimba za mapema.

Uchunguzi wetu wa kipekee unafichua kuwa mabadiliko ya tabia nchi kuwa sababu kuu inayochangia mimba za mapema na ndoa za mapema hasa kwa familia maskini zinazokabiliwa na baa la nja wakati huu wa ukame.

Ili kukabiliana na hali hiyo ya ukame , familia fukara zinazidi kuwaondoa binti zao shuleni na kuwaoza ili wapate fedha za kujikimu.

Katika kibanda kidogo katika kijiji cha Baha, binti mdogo aitwae Kadzo mwenye ujauzito wa miezi sita anaosha vyombo,huku akiwa anaimba nyimbo za kitamaduni.

Kwa mtazamo wangu,Kadzo anaonekana kuwa mwenye umri wa miaka 16, Lakini mume wake alisema ana miaka 18.Nilipojaribu kuomba vyeti vya kuzaliwa,mume wa Kadzo alisema,mkewe hana cheti hicho na pia hana kitambulisho cha kitaifa.

Kadzo na familia yake wanaonekana kuficha umri wake halisi. Kadzo anaonekana mchanga sana hivi kwamba itakuwa ngumu kuamini.

Haijalishi ni umri gani sahihi, Kadzo, kisheria, angali mtoto na ndoa za utotoni zimepigwa marufuku nchini Kenya tangu 1990, wakati nchi ilipoidhinisha Mkataba wa Haki za Mtoto, mkataba wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa wa kulinda watoto kutokana na unyanyasaji.

Kwa kuongezea Sheria ya Watoto ya 2001, Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ya 2006 na Sheria ya Ndoa ya 2014 (ambayo inakataza waziwazi ndoa za watoto walio na umri wa chini ya miaka 18), inakataza ndoa za mapema.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya nchini Kenya kati ya Januari na Februari 2022, wizara hiyo ilirekodi visa 45,724 za wasichana wajawazito wenye umri wa kati ya miaka 10 na 19.

Charity Mwaka mwanaharakati na mtetezi wa haki za watoto,anasema ni vigumu kwa viongozi kuripoti visa vya ndoa za mapema kwa sababu wengi wa viongozi wa eneo hilo wanatoka katika makabila sawa na familia za maharusi.

Ninapomuuliza Kadzo ikiwa alikubali mwenyewe kuolewa,anasema kuwa alikubali tu kuolewa ili tu familia yake ipate mali,angalau kufukuza ufukara unaoikabili familia hiyo,ufukukara uliosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Ikilinganishwa na mataifa mengine, Kenya iko juu katika safu ya nchi ambazo zinaweza kuhisi athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa. Mnamo mwaka wa 2018, Kielezo cha Global Adaptation Initiative cha Chuo Kikuu cha Notre Dame kiliorodhesha Kenya katika nafasi ya 36 kati ya nchi zote zilizo katika hatari ya kuathiriwa na athari za mabadiliko ya hali ya hewa-na ya 152 katika kujiandaa kukabiliana na athari hizi.

Wakati wa ukame wa 2020, wazazi wa Kadzo walimtoa shuleni na kumpa jukumu la kutafuta ajira za nyumbani. Lakini mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi huku eneo hilo likiendelea kukumbwa na ukame mwaka baada ya mwaka. Mbuzi wengi wa familia walikufa.Hatua iliyomfanya Kadzo kutafuta mume wa kumuoa ili wazazi wake wapate mbuzi wa kufuga.

Ulimwenguni kote, inakadiriwa wasichana na wanawake milioni 650 walio hai leo waliolewa wakiwa watoto, na kila siku, kwa wastani, wasichana wapatao 33,000 walio chini ya umri huo huozwa.

Madhara ambayo ndoa za utotoni husababisha kwa jamii na mataifa yote bado yanatathminiwa, lakini kadiri athari za mabadiliko ya hali ya hewa zinavyozidi kuongezeka duniani kote, wasichana kama Kadzo watakuwa katika hatari zaidi ya kuolewa wakiwa wachanga.

Bila uingiliaji kati kwa serikali, mashirika na wanaharakati, wasichana wengi zaidi wachanga katika nchi kote ulimwenguni wataolewa mapema kadiri hali ya joto duniani inavyoongezeka.

Wasichana ambao wameolewa mapema pia wana uwezekano mkubwa wa kuendeleza mchakato huo wa kijinsia isiyo ya kawaida na kusambaza kanuni hizi kwa watoto wao wenyewe, kulingana na ripoti ya Juni 2020 ya UNFPA.