Kutokana na unyanyapaa ambao bado unaendelea katika jamii,baadhi ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi hawataki kuonekana wakipata huduma na kufata dawa za ARVs katika kliniki za VVU.Walakini, dawa hizo ni muhimu sana kwa maisha na ustawi wao.

Ni mwendo wa saa nane mchana.Jua linaangaza miale kwenye milima na kuifanya kumeta kama almasi.

Milima na mabonde inavifanya vituo vya matibabu kuwa mbali hatua inayowafanya wanaoishi na VVU kushindwa kuhimili panda shuka ya milima hiyo pamoja na kuogopa unyanyapa na ubaguzi.

Lakini kwa Charo, mfanyakazi wa kujitolea wa afya ya jamii (CHV) ambaye ameishi na VVU kwa muda wa miaka 7, njia zinazopita katika milima zinamuunganisha na watu wanaoishi na VVU ambao anawapa ushauri wa kutokomeza msongo wa mawazo na unyanyapa na kuwapelekea dawa za ARV nyumbani kwao.

Kwa nyakati tofauti kila mwezi, yeye utembea kwa miguu kupitia milima hiyo,huku akichomwa na jua, akisafirisha dawa za kurefusha maisha (ARV) ambazo watu wanaoishi na VVU wanazitegemea ili kuishi.

"Sina baiskeli wala gari,natumia miguu yangu kuwafikia walengwa. Miguu yangu ni muhimu sana kwangu kwani inaniwezesha kuwafikia watu ninaowahudumia haraka. Ninatembea kupeleka dawa za kuokoa maisha za ARV kwa watu wanaoishi na VVU ambao wanazitegemea kwa ajili ya kuishi,” anasema Charo.

Charo anaeleza kuwa alipogundua kuwa ameathirika alidhani kuwa ndio mwisho wa maisha na alipitia unyanyapa kutoka kwa jamii,ila akashinda vita hivyo baada ya kujikubali.

"Nilipogundua kuwa nina virusi vya UKIMWI, niliogopa na kudhani kuwa ndio mwisho wangu. Lakini nilipona kwa ushauri na matibabu kwa kutumia dawa zilizopendekezwa za ARV. Pia nilipambana na unyanyapaa lakini niliweza kuushinda na kujieleza hadharani.Sasa ninaishi maisha yenye afya na furaha. Na hili ndilo ninalotaka kwa watu wanaoishi na VVU katika jamii yangu," anasema.

Licha ya changamoto anazokumbana nazo kama kukosa usafiri, Charo anajitolea sana kuwapa matumaini na kusaidia watu wanaoishi na VVU katika jamii yake.

"Kituo cha afya kiko mbali, jambo ambalo linawafanya baadhi ya watu kuwa na ugumu wa kuchukua dawa zao za ARV. Pia kutokana na unyanyapaa unaoendelea katika jamii, baadhi ya watu hawataki kuonekana wakipata huduma kwenye kliniki za VVU. Hivyo, najitwika jukumu la kupata tembe za ARV kutoka hospitalini na kuwapelekea,"anabainisha.

Kazi ngumu na kujitolea kwa Charo imesaidia kupunguza unyanyapa na pia baadhi ya wenye VVU sasa wamejikubali na kuanza mchakato wa kutumia ARV.

"Charo amesaidia sana watu kama sisi tunaoishi na virusi vya ukimwi, huwa anatutembelea na kuchukua muda kusikiliza shida zetu. Hii ina maana kubwa sana kwetu. Na tuna imani naye kwani anaelewa tunayopitia tangu atusaidie." pia anaishi na ugonjwa huo," anasema Fatuma ambaye ni miongoni mwa walionufaika na huduma za Charo.

Fatuma ambaye anasema baada ya kupata ushahuri kutoka kwa Charo,sasa amejikubali na ameanza kutembelea vituo vya afya kufata tembe za ARV.

"Nimejikubali na sasa nameza tembe za ARV,kinyume na awali ambapo ilikuwa simezi kwa sababu ilikuwa sijajikubali na niliogopa unyanyapa na kutengwa na jamii,"anaeleza Fatuma.

Pia anaongeza kuwa alifanikiwa kujifungua mtoto akiwa salama na yote hayo yanajiri baada ya kupokea ushahuri wa kimatibabu kutoka kwa Charo.

"Licha ya kuwa nimeathiri mimi na mume wangu,uzuri ni kwamba nilijifungua mtoto mwenye afya na asiyekuwa na VVU,yote haya ni baada ya kufuata ushauri niliopewa na afisa wa afya,"anasema Fatuma.

Kwa upande wake Tsuma ambaye alipata maambukizi hayo mwaka jana,anasema unyanya pamoja na msongo wa mawazo ndio ulimfanya kususia tembe za ARV,kwa kuhofia kukejeliwa na wanajamii.

"Niliogopa kufata dawa kwa sababu sikutaka kujulikana kuwa nimeathirka,huku kwetu ukijulikana uko na Ukimwi basi unatengwa na kukejeliwa kila uchao,"anasema Tsuma.

Lakini baada kutembelewa na Charo na kupewa ushauri,basi Tsuma alikujubali na kuanza kumeza dawa na kwa sasa anasaidiana na Charo katika kutoa hamasa mashinani.

"Kwa sasa nimeungana na Charo katika kutoa ushauri kwa waathiriwa wengine ambao hawajajikubali,"anasema Tsuma.

Takwimu za mwaka 2021 za kaunti ya Kwale zinaonyesha kuwa watu 18,140 wanaoshi na VVU,ambapo 16,950 wakiwa watu wakubwa huku 1,182 wakiwa watoto.

Kulingana na afisa anayesimamia maswala ya Ukimwi kaunti ya Kwale daktrari Fatihiya,wanawake wanaongoza kwa asilimia 4.6,huku wanaume wakiwa asilimia 1.9.

Tangu mwezi Septemba 2022, watu 13,609 wenye VVU wamenakiliwa kutumia ARVs,huku wagongwa 4,531wenye VVU hawatumii ARVs.Kuhusiana na swala hilo dkt.Fatihiya amesema msongo wa mawazo na unyanyapa huenda ikiwa sababu kuu zinazochangia kwa watu hao kutotfata ARVs.

"Wale ambao wamesusia dawa,wengi ni wale ambao hawajajikubali na pia wanakabiliwa na msongo wa mawazo na wanahofia unyanyapa katika jamii,"anasema Fatihiya.

Daktari Fatihiya ameongeza kuwa wanawake wanaogoza katika kutembelea vituo vya afya kutafuta ushauri na dawa za ARVs ikilinganishwa na wanaume.

"Idadi ya wanawake wenye VVU wanatembelea vituo vya afya kwa wingi kutafuta ushauri na dawa za ARVs ikilinganishwa na wanaume,"alisema Fatihiya.

Anasema wanajitahidi kupiga vita msongo wa mawazo na unyanyapa kwa watu wenye VVU katika jamii.

“Tunahakikisha tunatoa hamasa dhidi ya unyanyapa kwa watu wenye virusi vya Ukimwi,tutaiambia jamii kutowatenga kwani Ukimwi sio mwisho wa maisha”,alisema Fatihiya.