Kutokana na kukosekana kwa mazao, vifo vya mifugo, njaa kali na safari ndefu za kutafuta maji, wakazi wa  Kaunti ya Tana River Kusini Mashariki mwa Kenya, wanastahimili msimu wa nne wa kukosa mvua.

Huu ukiwa ni ukame mkubwa wa nne katika kipindi cha miaka kumi, pia ni ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa, lakini mbali na janga hilo,jamii inasimulia hadithi mpya ya ustahimilivu kutoka kwa msaada wa serikali na mashirika ya kiraia.

Katika kijiji cha Dayate , wadi ya Wayu kaunti ya  Tana River, mazizi ya ng’ombe matupu yanakukaribisha katika nyumba nyingi za jamii ya wafugaji.

Vyanzo vyote vya maji vimekauka na maeneo ya malisho ya mifugo hakuna, huku wafugaji wakilazimika kuhamisha mifugo yao kilomita zaidi ya mia moja hadi kwenye misitu na eneo la Tana Delta.

Bwawa la maji lililokauka

‘Nimepoteza karibu mifugo yangu yote, ng’ombe, mbuzi, kondoo. Kwa sasa tumebaki na mazizi matupu,’ Alisema Godhana Bodhole mwenye umri wa miaka 69.

Zizi la ng'ombe kijiji cha Dayate

Bodhole amekuwa mfugaji maisha yake yote. ‘Sijawahi kuona ukame unaokaa muda mrefu kama huu’, Aliongeza.

Jirani yake, Suleiman Abarufa, pia ni mfugaji. Alipoteza ng’ombe 38 wakati huu wa kiangazi. Alisema vyanzo vya maji ambavyo vinaptikana ni takriban kilomita 30 kutoka nyumbani kwake.

 “Baada ya ukame kudumu kwa kipindi cha misimu mine, nimabakia na mbuzi 2 nyeupe, hata hizo niko na bahati sana kuwa nazo,” Alisema.  

Kulingana na ripoti ya shirika la kijamii la mtandao wa kibinadamu kuhusu maeneo yaliyo kame , zaidi ya watu milioni 4.2 ikiwa ni sawa na asilimia 24 ya watu wanaoishi maeneo hayo kame kwa sasa wanakumbwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula huku watu milioni 2.7 wakihitajika kushughuliwa kwa dharura kutokana na shida wanazopitia.

Ripoti hiyo zaidi inasema kuongezeka kwa kasi hali ya ukame kunaongeza mazingira magumu kwa jamii kuweza kustahamili. Wakulima hasa katika maeneo hayo pia wameshindwa kupata mazao kwa misimu mitano mfululizo huku wafugaji nao wakipoteza zaidi ya mifugo milioni 2.4.

Lakini hakuna kitu kigumu kisicho na tumaini. Habari njema ni kwamba, serikali kwa ushirikiano na mashirika ya kiraia yameanzisha zoezi la kuwaepusha wafugaji kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame katika siku zijazo.

Mojawapo ya mipango hii ni ule wa kununua na kuuza mifugo ambayo imeshindwa kustahamili makali ya ukame. Mpango unaotekelezwa na serikali kwa ushirikiano na shirika la msalaba mwekundu nchini Kenya.

Katika mpango huo, mifugo inayotishiwa na ukame na uhaba wa chakula inanunuliwa kwa kima cha shilingi elfu kumi na tano,kiwango ambacho ni cha juu kulingana na soko la mifugo lilivyo kwa sasa.

Mifugo hiyo kisha huchinjwa na kusambazwa kwa familia ambazo zinakumbwa na uhaba wa chakula.

Baadhi ya mifugo iliyochinjwa

Mpango huu unanuia kupunguza hasara kwa jamii za wafugaji na kuziwezesha kununua mifugo mingine wakati ukame unapoisha.

“Hadi kufikia sasa tumenunua mifugo 1,255 katika magatuzi madogo 3,” Alisema  Bwana Gerald Bombe, ambaye ni afisaa mkuu mshirikishi wa shirika la msalaba mwekundu kaunti ya Tana River. 

Suleiman Abarufa, kutoka kijiji cha Dayate ni mmoja wa wafugaji walionufaika na mpango huo. 

“Niliuza ng’ombe moja kwa shilingi elfu kumi na tano, sasa niko na pesa ambazo naweza kununulia familia yangu chakula na pia kuwekeza kidogo ili ninunuwe ng’ombe zaidi mvua itakapoanza kunyesha,” Alisema. 

Galole Dhube, ambaye ni kiongozi wa vijana katika kijiji cha Wayu Duka pia amefaidika na mpango huo. Alisema baadhi ya mifugo yake ilipoteza hadi asilimia 90 ya ubora wa thamani ya soko.

 “Tunafurahia mpango huu, tunapunguza hasara za kupoteza mifugo kutokana na makali ya ukame, pia tunapunguza shinikizo hasa kwenye maeneo madogo ya malisho ambayo yamesalia,” Alisema. 

Kulingana na Bwana Bombe kuna zaidi ya ng’ombe 3,000 ambao bado wanahitaji kununuliwa kutoka kwa wafugaji kabla ya hali kuwa mbaya zaidi. Na zaidi ya mifugo 5,000 inayohitaji chakula kwa dharura.

“Tunahitaji kwa haraka chakula cha ziada kwa ng’ombe kabla mambo hayajaharibika,watu hapa wanategemea mifugo, ndio utajiri wao,” Alisema.

Eneo la bahari Tana Delta

Ikumbukwe kuwa tangu jadi, mifugo katika kaunti ya Tana River hulisha ndani ya vyanzo vya maji katika eneo la Tana Delta wakati wa kiangazi, na kurudi nyumbani wakati wa msimu wa mvua ili kutoa muda kwa nyasi kumea tena katika eneo hilo la Delta.

Lakini kutokana na ukame ambao umeshuhudiwa mara kwa mara, eneo hilo la Delta pia linalishwa mifugo kupita kiasi hivyo kuwa vigumu kurudisha hali yake ya kawaida kutokana na hali ya ukame inavyozidi kuwa mbaya.

Mfugaji wa Tana Delta

Kutokana na hilo basi, wafugaji sasa wameanza kuja na mbinu mbadala za malisho ili kupunguza shinikizo kwenye mfumo wa ikolojia. Ambapo wakulima kandokando ya mto Tana hulima mahindi na wanapovuna huwauzia wafugaji mabua ya mahindi ili kulisha ng’ombe zao.

 “Mabua ya mahindi ni kama mkombozi kwetu wafugaji,unaweza kuyahifadhi kwa urahisi na kwa muda mrefu na kwa sasa ndio tunatumia kulisha mifugo yetu iliyobaki hapa,” Alisema Suleiman Abarufa kutoka kijiji cha Dayate.

Mbali na juhudi hizo za wanajamii, uongozi wa serikali ya kaunti ya Tana River pia unafanya kazi na jamii kubuni miradi itakayodumu kwa muda mrefu. Miradi ambayo itawapatia lishe mifugo misimu yote.

Wafugaji kutoka Dayate

Nzioka Wambua, ni mkurugenzi mkuu wa idara ya mifugo katika kaunti ya Tana River. Alisema wameanzisha mradi wa upanzi wa nyasi kandokando ya mto. Nyasi hizo zitavunwa na kuwekwa katika maeneo salama na kutumiwa kama chakula na mifugo wakati wa kiangazi.

“Tunafanya kazi na vikundi vya wakulima visivyopungua 100 ambavyo vimepatiwa mafunzo kuhusu kulima,kuvuna na kuhifadhi nyasi,”  Alisema, akiongeza kuwa lengo ni kuhakikisha hakuna mifugo itakayokufa siku za usoni kutokana na athari za ukame.

“Hii ni hatua ya mpango wa muda mrefu ya kuhakikisha kuwa vifo vya mifugo ni jambo ambalo tutalisahau kabisa,” Alisema.  

Shirika la msalaba mwekundu Kenya tayari limeanza kutekeleza mpango huo wa kununua mifugo katika kaunti jirani ya Kilifi ambapo baadhi ya wafugaji wanapitia hali ngumu kutokana na ukame.

Aidha mipango kama hiyo inalenga kujenga uwezo wa wafugaji kustahimili ukame  na kutoa fursa ya kupunguza kwa kiasi kikubwa hasara za kijamii, kiuchumi na kibinadamu wakati wa ukame.

Ikiwa ni pamoja na kusaidia maisha ya viumbe hai, maji na uhaba wa chakula pamoja na tabia ya wafugaji kuhama ambayo huenda ikasababisha migogoro ya kiuchumi kutokana na rasilimali chache.