Kunawiri kwa Mahindi na mboga ni taswira iliyonikaribisha katika mashamba ya wanajamii wa kijiji cha Mwalewa  kinachopakana na msitu wa Gonja eneo la Lungalunga kaunti hii ya Kwale.

Mimea ya mboga kama vile mchicha, biriganya na tomato zimenawiri kwa rangi ya kijani kibichi ishara kwamba wakulima wanatarajia kuvuna mazao mengi na yenye afya.

Lakini kulingana na wakulima eneo hilo,hali haikuwa hivyo miaka kadhaa iliyopita kutokana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Ambapo hali ya kiangazi ilishuhudiwa kwa muda mrefu.

Hamadi Bakari ambaye ni mwenyekiti wa kijiji hicho alieleza kuwa awali kutokana na kudorora kwa ukulima baadhi ya watu waliendeleza ukataji wa miti msituni ili kukimu mahitaji ya familia zao.

Wakulima hao sasa wameunda kikundi ili kwa pamoja waweze kuhifadhi msitu wa Gonja kutokana na uharibufu.

Ni kupitia juhudi zao za uhifadhi wa msitu waliweza kutambulika na kupata mafunzo ya ukulima wa kisasa kupitia ufadhili wa shirika la kimazingira la WWF-Kenya.

Sasa wakulima wamelazimika kubadili mbinu za kilimo ili kupata mazao.

Wakulima wamekumbatia kufanya kilimo kwa kutumia mbinu za kisasa ikiwemo kunyunyizia mashamba maji.

Mto Umba ulioko mita chache kutoka kijiji hicho unawatosheleza wakulima hao ambao wanayatumia maji ya mto huo kuendeleza ukulima wa unyunyiziaji maji. 

Mariam Bakari pia ni mkulima eneo hilo, alisema hawakuwa na budi ila kutumia mbinu za kisasa ili kufufua kilimo na kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Bi Bakari sasa anatambua fika umuhimu wa kuendeleza kilimo Kwa kutumia mbinu za kisasa.

Katika shamba lake kuna mchanganyiko wa mimea, anaendeleza kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.

Vilevile niliweza kukutana na mzee Mwanamwenga Chigamba kutoka kijiji cha Gandini, Kinango kaunti ya Kwale, eneo ambalo limetambulika ulimwenguni kutokana na kiangazi kikali.

Unapofika shambani mwake unakutana na mashimo yenye umbo la mraba yaliyopangwa sambamba.

Mbinu hii ya upanzi katika mashimo inafahamika kama Zai pit. Mkulima huanza kwa kuchimba mashimo yenye upana wa sentimita 20 hadi 40 na kina cha sentimita 10 hadi 20, lakini hutofautiana kulingana na aina ya udongo.

Mashimo hayo hujazwa matandazo,mbolea na mchanga ili kuongeza rutuba kwenye ardhi, pia yana uwezo wa kuzuia maji na ni bora katika kuzuia mbegu kusombwa na maji yanayotiririka.

Mzee Chigamba anaeleza kuwa kutokana na mvua chache eneo hilo la Kinango mbinu hiyo ya upanzi katika shimo lilliochimbwa na kutayarishwa kiustadi ndio suluhisho. 

Kwake shambani anapanda mimea yenye mavuno mengi kwani anatumia mbegu zinazostahimili ukame.

Pia anafanya mzunguko wa mimea yaani anabadilisha mara kwa mara aina ya mimea anayopanda.

Mbinu anazosema hufanya ardhi  kuwa na rotuba na hivyo kuwa na uhakika wa mavuno ya kutosha.

Mzee Chigamba alieleza  kuwa katika msimu uliopita aliweza kupata mazao marudufu kutumia mbinu za kilimo za kisasa. 

Zaidi Chigamba alieleza kuwa ingawa Kinango hukumbwa na kiangazi kikali kwake nyumbani hakuna njaa kwa sababu mavuno anayopata yanatosheleza familia yake wake wanne na watoto 27 uhakika wa chakula cha kutosha. 

Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, mashirika mbalimbali pamoja na serikali yamekuja pamoja na kuandaa muongozo kwa wakulima.

Kaunti ya Kwale ikishirikiana na shirika la WWF-Kenya wameamua kusaidia jamii kuendeleza ukulima wa kisasa.

Lance Mwadiga ni afisaa wa kilimo kutoka gatuzi la Kwale anaeleza kwa ufasaha kuhusu ukulima wa mbinu za kisasa walizoelimisha baadhi ya wakulima wa Kinango na Lungalunga, maeneo ambayo hukumbwa na kiangazi kikali kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Sasa wakulima wana matumaini makubwa kwa kuwa wamepatiwa ujuzi wa mbinu za kisasa za kilimo na hivyo kuwa na uhakika wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, suala ambalo linachangia pakubwa wao kutoingia katika misitu na kuendeleza uharibufu wa misitu hiyo.

Kulingana na ripoti ya mamlaka kuu duniani ya kushughulikia mazingira, UNEP Katika mwaka wa 2022, athari mbaya za mabadiliko tabianchi zilisababisha changamoto za aina tatu duniani zilizidisha na kuleta kuongezeka kwa ukosefu wa usawa, mizozo na kupanda kwa bei ya chakula na nishati.

Masuala yanayoweka wazi kuwa ipo haja ya kuchukua hatua za kushughulikia uhifadhi wa mazingira.

Hivyo kushinikiza mataifa kuweka kipaumbele mikakati ya kulinda mazingira ili kupata suluhisho endelevu kwa manufaa ya mwananchi.