Ni furaha kwa mvuvi pale anapovua samaki wa kutosha,Ila pale samaki anapokua haba baharini mvuvi hukosa amani na maswali kuibuka ni nini haswa kinachosababisha samaki kupungua.

Zipo sababu nyingi, kwa mfano ,wavuvi wa kijiji cha Dziphani ambao wapo katika kikundi kinachotoa ulinzi baharini- Bonje BMU, uharibufu wa mikoko ni moja wapo ya sababu hizo.

Mikoko huwa mazalia ya samaki na huwa kama kinga dhidi ya dhoruba, mmomonyoko wa ardhi na mafuriko. Pia husafisha hewa mara tano zaidi ya misitu ya nchi kavu kwani huhifadhi kaboni zaidi.

Kulingana na mwenyekiti wa kikundi hicho Saidi Chirunga uharibufu umetekelezwa na wakaazi wanaokata mikoko kwa matumizi yao binafsi pamoja na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za elnino miaka iliyopita.

Visiki vya miti ya mikoko katika eneo hilo vimetapakaa vikiashiria wazi uharibifu uliotokea.

Ili kupunguza athari zaidi, kikundi cha wahifadhi wa jamii huko Bonje kimekuja pamoja na kushirikiana na shirika la kimazingira la WWF-Kenya, idara ya misitu nchini na taasisi ya utafiti wa bahari KMFRI kurejesha maeneo ya misitu ya mikoko iliyoharibiwa.

Kikundi hicho cha Bonje kina  wanachama 1,200 kinajumuisha wavuvi, wachuuzi, na kina mama wanaokaranga na kuuza samaki.Wanachama hao huuza miche na kupanda upya mikoko kwani faida yake wanaitambua, zaidi ni kupunguza athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi.

Mbali na kurejesha hali kama ilivyo kuwa awali ili kuongeza idadi ya samaki eneo hilo, upandaji upya wa mikoko katika maeneo yaliyoharibiwa unalenga kusaidia kizazi kijacho.

Baadhi ya wavuvi wamelazimika kuacha uvuvi na kutafuta njia mbadala za kujikimu kimaisha  kutokana na hasara ya kukosa samaki.Hii ni kwasababu samaki wamepungua kwa kiasi kikubwa baharini.

Aidha Chirunga ameweka wazi ardhi eneo hilo haifai kwa kilimo kutokana na mafuriko ya bahari na ukame wa muda mrefu unaokumba sehemu nyingi za Kinango kaunti ya Kwale, hivyo basi ikawalazimu kukumbatia upandaji mikoko.

Mkereketwa huyo wa mazingira amesema wanalenga kufikia mafanikio ya kiuchumi na kimazingira kupitia uhifadhi endelevu.

Ameongoza kuwa tangu mradi huo uanze mwaka 2018, matumaini kwa jamii inayotegemea uvuvi yamefufuliwa kwa kiasi kikubwa. 

Ili kuimarisha uhifadhi katika eneo hilo, kikundi cha Bonje BMU kimetumia baadhi ya ardhi kuwa mabwawa ya ufugaji samaki.Aina ya samaki wanaofuga ni pamoja na tilapia, mborode na kambakamba.

Chirunga anaeleza kuwa mradi wa ufugaji samaki umebadilisha kabisa maisha yao kwani wenyeji wamepata kuongeza mbinu nyingine za kujipatia riziki badala ya kuendeleza uharibufu wa mikoko.

 

Ameongeza kwamba shughuli wanazoendeleza zimechangia pakubwa uwajibikaji katika jamii na kuunda fursa za ajira kwa vijana wasio na kazi.

Mbali na upanzi wa mikoko pamoja ufugaji samaki wanajishughulisha na uuzaji wa miche ya mikoko jambo ambalo amelitaja kuwaingizia fedha za kuhudumia familia zao.

Katibu wa kikundi hicho Mariam Konde aliweka wazi kuwa uhifadhi wa Mikoko umewasaidia kupata riziki na kusaidia familia zao.

Bi Konde aliaeleza kwamba mradi huo umeimarisha usalama katika eneo hilo huku vijana wengi wakiingia kwenye uhifadhi na kutumia nguvu zao kuleta mabadiliko katika jamii.

Katibu huyo anasema mpango wa kurejesha hali ya mikoko umeleta furaha katika maisha yao kwani mazingira yanarejea katika hali yake ya asili.

Wanaimani kuwa kuendeleza kuipanda upya mikoko kutapunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha maisha.

Mariam Konde.Katibu wa Bonje BMU.

Bi Konde alionyesha matumaini kuwa mustakabali wa wanawake na watoto katika eneo hilo utakuwa mzuri zaidi pindi mradi huo utakapokuwa na mafanikio kwa sababu wao ndio walioathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi.

Nilitaka kujua ni vipi yeye kama mwanamke anaweza kutimiza kazi zake nyumbani na kuendeleza shughuli ya uhifadhi wa mikoko?

Aidha alieleza kuwa kikundi chao hukumbwa na changamoto kwani baadhi ya wakaazi wamepuuza agizo la kutokata mikoko na hivyo basi kuzorotesha juhudi zao za uhifadhi.

Suala ambalo wanakabiliana nalo kikamilifu kwa usaidizi na shirika la uhifadhi wa misitu nchini kwa kupiga doria.

Kwa upande wake Mratibu wa shirika la kimazingira la WWF Mohammed Pakia alieleza kuwa kama shirika wamejizatiti kusaidia jamii ikiwemo kikundi cha Bonje BMU kupitia miradi inayolenga uhifadhi wa mazingira.

Vilevile kuwajengea uwezo wakazi katika kufanya uvuvi endelevu pasi kufanya uharibufu.

Ni wazi kuwa upanzi na uhifadhi wa mikoko ni moja wapi ya suluhu ya kukabiliana na mabadilko ya tabianchi hasa katika mazingira ya baharini.