Katika kijiji cha Mikomani eneo bunge la Rabai kaunti ya Kilifi,nakutana na Juliana Fondo.Yeye ni mfugaji. Boma lake limezungukwa na mabanda anayotumia kufuga ng’ombe,kuku na kanga.

Kinyesi cha ng’ombe anachopata kutoka kwa ng’ombe wake 6 anaofuga anasema ni dhahabu kwake.Anatumia kinyesi hicho kutengeneza gesi asilia yaani Biogas anatumia kwa upishi.

“Biogas imerahisisha kazi yangu,ni safi, haitoi moshi na ninaweza kupikia wakati wowote bila kuogopa kwamba itaisha.Inaweza kutumika kwa saa nane mfululizo.Ninaitumia kupika chakula cha familia yangu ya watu watano,” Alisema Bi Fondo.

“Endapo kila boma liko na mbinu hii ya kupata gesi asilia na kupikia,basi hatutashuhudia uharibifu mkubwa wa misitu ambao tunashuhudia kwa sasa,” Aliongeza Bi Fondo.

Wizara ya kawi kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Kilifi ilimfadhili Bi Fondo kujenga mtambo huo wa kutengeneza gesi asilia. Mtambo ambao ulijengwa kwa kipindi cha mwezi mmoja,na kwa sasa amekuwa mfano wa kuigwa na jamii kwani watu wengi huzuru boma lake kujifunza.

“Kwa wiki naweza kupokea wageni angalau wawili kila mwezi ambao hutaka kujua jinsi ya kutengeneza, na kutunza mtambo huu wa gesi asilia,”Alisema Bi Fondo.Kabla Bi Fondo aingilie upishi wa kutumia gesi asilia, alisema alikuwa akitumia muda mwingi kwenda msituni kutafuta kuni.Huku mara nyengine akilazimika kununua miti kwa ajili ya kukatwa na kutengeneza makaa. Shughuli iliyomgharimu pesa chungu nzima.

Juliana Fondo akiwa jikoni kwake.

Bi Fondo ametumia gesi hiyo kwa muda wa miaka mitano sasa. Hivyo kumpa yeye wakati mzuri wa kufanya kazi nyengine za nyumbani kikamilifu bila kuwa na wasiwasi wa kutafuta kuni ama makaa.

“Ikiwa serikali itasaidia wafugaji kujenga mitambo ya kutengeza gesi kutumia kinyesi cha mifugo, basi itasaidia sana kwani kutakuwa hakuna uharibifu wa ukataji miti kwa matumizi ya makaa ama kuni,hivyo basi tutakuwa tunalinda mazingira,”Alisema Bi Fondo.

Mkorogo wa kinyesi cha ng'ombe:Picha na Captain Nyota

Bi Fondo alisema huwa inamuuma sana anapoona watu wanaharibu misitu kwa kutafuta kuni ama makaa.Na tabia hiyo ndio imeleta tatizo la mabadiliko ya tabianchi tunayoshuhudia kwa sasa.

“Mimi hupanda miti na mara kwa mara nawasihi watu kupanda miti. Huwa inanisumbua akili ninapofikiria kwamba siku moja misitu yetu ya Kaya itaisha na hatutakuwa na kitu cha kujivunia na kuonyesha vizazi vijavyo,”Alisema Bi Fondo.

Katika kijiji jirani cha Makobeni,nakutana na Selina Juma. Yeye ni mwenyekiti wa kikundi cha Chauringo-Makobeni Dairy. Kikundi ambacho kinajishughulisha na maswala ya ufugaji wa wanyama.

Awali, Bi Juma alikuwa akitembea mwendo wa zaidi ya saa sita hadi msitu wa Kaya ulioko karibu naye ili kutafuta kuni za kupikia.Shughuli ambayo kwake haikuwa inamaliza muda wake pekee bali ulimuweka katika hatari ya kudhulumiwa kijinsia njiani.

Bi Juma alionyesha shukrani zake kwa shirika la Climate Action Plan, ambalo lilimfadhili na kujenga mtambo mdogo wa kutengeza gesi asilia kwa kutumia kinyesi cha ng’ombe wake wawili anaofuga.

Selina Juma akiwa shambani

“Biogas ni ya muhimu sana kwangu,inarahisisha mambo yangu hata ninapotoka kwenda shughuli zangu sina wasiwasi kwasababu mume wangu anaweza kuwasha na kujipikia chakula.Pia kwa kutumia mbinu hii ya upishi siharibu mazingira kwa kukata miti,” Alisema Bi Juma.

Bi Juma mwenye umri wa miaka sitini alisema utumiaji wa mbinu hiyo safi ya upishi umemfanya kuimarika kiafya,kwani mbali na kuwa hafanyi kazi ngumu ikiwemo kutafuta kuni pia havuti moshi wa kuni na makaa anapopika.

“Endapo wanawake watapata muda mzuri wa kupumzika na wala sio kutembea mwendo mrefu kutafuta kuni na maji basi wengi wetu tutakuwa na afya njema na kuishi maisha marefu.Hivyo nawasihi wanawake wawekeze katika ufugaji na kujenga mitambo ya kutengeza biogas na kuwacha kukata miti ili kulinda mazingira,’Alisema Bi Juma.

Hata hivyo kina mama hao wanazo changamoto wanazopitia katika kutengeza na kutumia gesi asilia.Kwa mfano,uhaba wa maji unaoshuhudiwa katika maeneo mengi eneo hilo la Rabai umewapatia wakati mgumu kupata maji yakutosha kukoroga kinyesi hicho cha ng’ombe.

Pili,kutokana na mabadiliko ya tabianchi ,kunashuhudiwa kiangazi ambacho kinawaathiri ng’ombe kwani hawapati chakula cha kutosha ambacho kitawawezesha kutoa kinyesi kingi,ambacho ndio muhimu kwa utengenezaji wa gesi asilia.

Ili kutengeneza gesi asilia,wanawake hao hukusanya kinyesi cha ng’ombe kutoka kwenye sehemu za malisho,kisha huweka kwenye chumba kidogo cha kuchanganya kinyesi na maji. Wanasaga kwa kutmia mikono mpaka mkrogo huo umwe laini kabisa.

Kisha kinyesi huruhusiwa kuingia ndani ya mtambo wa kutengeneza gesi asilia ambayo inaweza kuwaka.Kisha gesi hupitishwa hadi nyumbani kwa kutumia mabomba ambapo huunganishwa na jiko tayari kwa kuwasha na kupika.

Hatimaye tanki hukusanya uchafu ambao umetumiwa kuzalisha gesi asilia. Taka hiyo baadaye hutumiwa kama mbolea.

Kulingana na utafiti wa shirika la Poor People’s Energy Outlook 2019, kwa wastani mtu hutumia saa tano na dakika 16 kwa siku kukusanya na kuandaa kuni na mafuta ya kupikia. Hivyo kubadilisha hadi kutumia mbinu safi ikiwemo gesi asilia kutapunguza muda huo hadi saa tatu na dakika 18 kwa siku.

Mkurugenzi mkuu wa idara ya kawi kaunti ya Kilifi Wilfred Baya alisema wametoa mafunzo kwa Zaidi ya vijana na wanawake 100 katika maeneo bunge yote 6 kaunti ya Kilifi ili kukumbatia mbinu safi za kupika hasa kwa kutumia gesi asilia na makaa yanayotengenezwa kwa kutumia bidhaa za mnazi.

“Tangu tuanze kuhamasisha jamii kutumia mbinu safi za kupika mwaka wa 2018, kiwango cha uharibifu wa miti imepungua kwa asilimia kumi,”Alisema Baya.


Brian Murumba,afisaa wa mawasiliano kutoka Clean Cooking Association of Kenya (CCAK) amesema hadi kufikia sasa wamehamasisha Zaidi ya wanawake 70 kutoka kaunti ya Kilifi kuhusu mbinu safi za upishi.

Hii ikiwa ni miongoni mwa miradi iliyodhaminiwa na Worldwide Fund for Nature (WWF-Kenya) kutekeleza mbinu za kijamii za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Lengo moja kuu ni kuhakikisha kuwa wanawake wanatumia takataka na kuzalisha nishati ya kupikia au ya kutumia nyumbani ili kupunguza utoaji wa hewa kaa na kuboresha maisha ya familia,” Alisema Murumba.

Profesa Bernard Fulanda mtaalamu wa maswala ya sayansi ya Bahari na mabadiliko ya tabianchi alisema mbinu ya upishi safi husaidia katika kupunguza utoaji wa hewa kaa.

“Utoaji wa hewa kaa unaweza kupungua kwa viwango tofauti kulingana na matumizi ya nishati safi.Baadhi wanaweza kupunguza hadi asilimia mia moja,lakini kwa wastani inaweza kupunguzwa kwa asilimia 60-70,”Alisema Profesa Fulanda.

Habari hii imefanikishwa kwa usaidizi kutoka kwa WWF-K VCA Project na MESHA