Hamisa Zaja ni mkurugenzi mtendaji wa shirika linalowahudumia watu wenye ulemavu eneo la Pwani –Coast Association for Persons Living with Disability.

Nilikutana naye kwa mahojiano, katika ofisi yake iliyo katika mtaa wa Majengo eneo bunge la Mvita, kaunti ya Mombasa. Shirika hilo husaidia kutafuta suluhu kwa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu.

Ujio wa virusi vya corona humu nchini ulizua wasiwasi mwingi kwa jamii. Zaidi ni kwa watu walio na mahitaji maalum ambao hadi kufikia sasa baadhi yao wangali wanakumbwa na changamoto za kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Shirika la Afya Ulimwenguni -WHO, lilitoa muongozo wa jinsi watu wanavyoweza kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, ikiwemo kuosha mikono kwa maji na sabuni kwa angalau sekunde 20, kukaa umbali wa mita moja unusu na mtu mwingine, pamoja na uvaaji wa barakoa.

Uvaaji Wa Barakoa

Uvaaji wa barakoa mara nyingi umehusishwa na watu wanaofanya kazi hospitalini, hivyo ilikuwa jambo geni kwa mtu wa kawaida kuvaa barakoa. Na kwa mara ya kwanza kila mtu uliyepishana naye alikuwa amevalia barakoa ili aweze kuepuka maambukizi. Mashirika mbalimbali na wafadhili wakajitolea kutoa barakoa kwa umma.

Lakini barakoa nyingi zilizotengezwa, zilizotolewa na hata kununuliwa, hazikutilia maanani watu walio na ulemavu wa kusikia na kuzungumza. Hivyo kutatiza mawasiliano kati ya watu hao.
Kwa kawaida jamii hiyo hupata taarifa kwa kutumia ishara na kusoma midomo, hivyo basi wanapovaa barakoa za kawaida ambazo hufunika hata mdomo, huwa vigumu kwao kuelewa kinachozungumziwa na kuelewa ujumbe unaotolewa.

Changamoto hiyo ikawa moja wapo ya shinikizo zilizomfanya Hamisa Zaja kubuni barakoa maalum kwa watu wanaoishi na ulemavu wa kusikia na kuzungumza.

Shirika hilo liligawanya barakoa hizo kwa watu wanaoishi na ulemavu wa kusikia na kuzungumza katika sehemu mbalimbali nchini.

Ann Otum ni mama ambaye mwanae Teddy Otum mwenye umri wa miaka 27, alifaidika na barakoa hizo.

Alinieleza kuwa maisha ya mwanawe yalisimama kwa muda pindi kisa cha kwanza cha virusi vya corona kilipobisha hodi humu nchini,kwani kwa kuvaa barakoa za kawaida za kufinika mdomo hangeweza kuwasiliana vyema na wenzake.

Na pia asipovaa barakoa anajiweka katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi hivyo.Hivyo ilimlazimu kubaki nyumbani na kukosa kutangamana na rafiki zake.

Ann alinieleza tangu mwanawe apate barakoa hizo, mawasiliano baina ya mwanawe na wenzake yameimarika si haba.

Nje ya jumba la shughuli nyingi la bima ya afya NHIF jijini Mombasa, nilikutana na Rashida Akinyi. Akiwa mjane na watoto watano, Rashida anafanya biashara ya kuuza nguo za kushona na uzi na bidhaa nyingine.

Ni kazi ambayo ameifanya kwa miaka 17 sasa. Kwa kipindi hicho cha miaka 17, kwa mara ya kwanza Rashida alilazimika kufunga biashara yake kwa miezi kadhaa. Hii ni baada ya serikali kutangaza kupatikana kwa virusi vya corona humu nchini.

Akiwa anaishi na ulemavu wa kusikia na kuzungumza, ilinibidi nitafute usaidizi wa mkalimani ili tufanikishe mahojiano yetu.

Rashida alinieleza kuwa kwa siku yeye huhudumia zaidi ya watu 500. Hivyo alihisi kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi vya corona kwa sababu ya ukosefu wa barakoa ambazo zingeweza kumlinda na kwa wakati huo huo awasiliane vyema na wateja wake.

“Kwa kweli corona iliporitiwa humu nchini nilishikwa na uoga,na nikafunga biashara yangu, ukosefu wa barakoa pia ulichangia mimi kufunga biashara yangu kwasababu nilihisi siko salama kabisa,” alisema Rashida.

Akiwa mmoja wa waliofaidika na barakoa kutoka kwa Hamisa, Rashida ananiambia sasa anahisi kuwa salama anapovaa na kuhudumia wateja wake.

Shirika la Afya Ulimwenguni –WHO lilitoa wito kwa mataifa mbalimbali kuhamasisha umma umuhimu wa uvaaji wa barakoa pale ambako kiwango cha maambukizi ni kikubwa hasa kwenye mikusanyiko ya watu.

Kwa kuzingatia hilo, msaada huo wa barakoa maalum kwa watu wanaoishi na ulemavu wa kusikia na kuzungumza uliwafikia baadhi ya waumini katika kaunti za Kilifi, Kwale na Taita Taveta kupitia kanisa Katoliki jimbo la Mombasa.

Lilian Japani ni msimamizi wa Tume ya Haki na Amani Jimbo Kuu la Mombasa la kanisa Katoliki, tume iliyojumuishwa katika kamati ya masuala ya dharura ya kushughulikia janga la virusi vya corona katika jimbo la Mombasa.

Alisema mbali na bei ya juu ya barakoa, ukosefu wa barakoa maalum kwa walemavu, jamii hiyo ilihisi kutengwa kwa njia moja ama nyingine. Alisifia ubunifu wa barakoa hizo jambo ambalo alisema halikuwa limefikiriwa na mtu yoyote.

Teresia ni fundi anayezishona barakoa hizo. Katika ukumbi wa nyumba anayoishi anaendeleza ushonaji wa barakoa hizo. Alisema kuzishona kunahitaji umakini wa hali ya juu ili ziweze kufikia kiwango hitajika.

Anasema kwa siku anaweza kutengeneza hadi barakoa 40.

Hamisa Zaja amepokea tuzo kutoka kwa mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Ikiwa ni kutokana na juhudi zake za kuwasaidia watu wanaoishi na ulemavu wa aina yoyote ile bila kubagua.

Akiwa ndiye aliyebuni barakoa hizo, anasema amepokea uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa jamii, na hata kuvutia watu wengine wanawake ambao wamekuwa wakiagiza kutengezewa barakoa hizo kwa maswala ya urembo.

Zaidi Hamisa alisema watu wanaoishi na ulemavu wa kutoweza kusikia au kuzungumza walikuwa wameachwa nyuma wakati serikali ilipokuwa ikitoa msaada janga la corona lilipobisha hodi humu nchini, Hivyo ikawa kichocheo zaidi kwake kutengeneza barakoa hizo ili ziweze kuimarisha mawasiliano.

Anasema hadi kufikia sasa amesambaza zaidi ya barakoa 3,000 huku akipata maombi kutoka kaunti mbalimbali humu nchini na hata mataifa ya nje.

Faiz Mohammed Shee ni mwanasayansi na mtafiti kuhusu maswala ya virusi, Anasema kuna vigezo vya kuzingatiwa kwa utumiaji wa barakoa salama.

Huku akisifia ubunifu huo ambao anasema ni wa kuigwa ili jamii ya watu wanaosihi na ulemavu huo wa kuzungumza na kusikia wahisi kwamba hawajawachwa nyuma katika vita dhidi ya corona.

“Barakoa nzuri ni iwe hairuhusu virusi kuingia ama kutoka, muhimu zaidi ni kuingia kwasababu unajikinga wewe kwanza kabla ya wengine, alafu pia iwe ya kitambaa ambacho mtu anaweza kupumua kwa urahisi akiwa ameivaa. Kama barakoa hizo zina vigezo hivyo, basi ni ubunifu mzuri ambao unafaa kuigwa”, Alisema Faiz.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa jumla ya watu 918,270 wanaishi na ulemavu wa aina mbalimbali humu nchini.

Huku zaidi ya watu 250,000 katika idadi hiyo wakiishi na ulemavu wa kutozungumza na kusikia.

Picha - Development Initiatives based on KNBS



 


 

More Stories

Buriani jenerali Francis Ogolla

Idara ya polisi yasema mgomo wa madaktari ni usumbufu

Seneta Miraj amtetea waziri wa afya

Bandari ya Lamu kuipiku ile ya Mombasa asema Mbogo