Fatuma Tabu Kibango alipoolewa na kuanza maisha mapya katika kijiji cha Magwede kaunti ya Taita Taveta, hakuwa na ufahamu kuwa ameanza maisha ya kukesha usiku kucha akilinda mazao yake yasiharibiwe na wanyamapori.

Fatuma alizaliwa na kulelewa katika kijiji cha Mackinon kipatikanacho katika barabara kuu ya Mombasa –Nairobi. Takriban kilomita sitini hadi kijiji cha Magwede. Kijiji ambacho kimepakana na ranchi ya Rukinga kaunti ya Taita Taveta.

Tatizo la wanyamapori kuingia katika mashamba ya watu katika kaunti hiyo limekuwa kero kwa wakazi wa eneo hilo kwa miaka mingi.Mzozo kati ya wanyama pori hususan ndovu na wakazi hao limefanya watu wengi kupoteza maisha, kujeruhiwa na hata mimea kuharibiwa.

Mzozo ambao kwa kiasi kikubwa umesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi. Ukataji wa miti na uharibifu wa rasilimali umesababisha mabadiliko mengi ya tabia nchi, na kusababisha kukauka kwa vyanzo vya maji na pia kuleta mvutano wa rasilimali kati ya wanyama pori na binadamu.

Hali ambayo imesababisha wanyamapori kuhama makazi yao na kuingia katika mashamba ya binadamu.Wakulima, wakilazimika kukesha usiku kucha ili kulinda mazao yao yasiharibiwe na wanyamapori hasa ndovu.

Kama anavyosimulia Fatuma Tabu Kibango mama wa watoto 6.

 

Ni hali ambayo mama Umazi Mwaruwa Makutu, mama wa watoto 3 kutoka kijiji cha Buguta kaunti hiyo ya Taita Taveta anapitia. Alisema kero la ndovu limekuwa likisababisha yeye na wanawe kutoa mazao yao shambani yakiwa machanga ili yasiharibiwe na ndovu.

‘Sisi ni majirani na wanyama pori .Ukiona ndovu amekula mazao ya mwenzako unavuna yako kama hayajakomaa, kama pojo tunavuna kama hazijaiva kikamilifu alafu tunahifadhi mbegu,’ Alisema Umazi.

‘Alafu tunapanda mbegu changa ambazo haziwezi stahamili ukame,zikipata jua kidogo zinanyauka kwa sababu zilivunwa zikiwa bado hazijakomaa’, Umazi aliongeza kusema.

Umazi Mwaruwa akiwa shambani Kwake.

Peter Musyoki ni mkulima kutoka kijiji cha Ngambenyi eneo la Kasigau. Anamiliki shamba la ekari 6 na yeye hufanya kilimo biashara. Musyoki alisema kuwa ndovu wamekuwa kero kubwa kwao.

Alisema kuwa wanalima lakini huwa hawana uhakika wa kupata mazao. Kwani mara nyingi ndovu huvamia mashamba yao ghafla.

‘Tunalima lakini kuvuna ni shida kwani hatuna uhakika wa kupata mazao, kuna wakati tulilima na ndovu wakatokea ghafla usiku, tulipoamka tulipata mahindi yote yameliwa,’ Alisema Musyoki.

Ili kutatua tatizo hilo, mtafiti wa kisayansi Simon Kasaine, alivumbua singe’nge inayotengenezwa kwa mabati madogo madogo ambayo hufungwa kwa kamba na kuzungushwa katika mpaka wa shamba.

Mabati hayo madogo yanapogongana hutoa sauti inayotishia ndovu na wakati wa usiku mabati hayo yanang’aa kiasi cha kuwatishia ndovu wasifikie mashamba hayo.

Singe’nge hiyo imepewa jina la mtafiti huyo wa kisayansi anayefanya kazi na shirika la Wildlife Works huko Maungu kaunti ya Taita Taveta, KASAINE FENCES.

Huyu hapa Kasaine akinielezea kwa undani kuhusiana na singe’nge hiyo.

 

Fatuma Tabu Kibango ambaye alilazimika kukesha usiku kucha kulinda mazao yake yasiharibiwe na ndovu, alinieleza kuwa kwa sasa anapata angalau lepe la usingizi.

Akiwa mmoja wa wakulima ambao wamefaidika na singe’nge hiyo ya Kasaine, alisema sing’enge hiyo imepunguza sana ndovu kuvamia shamba lake la ekari moja.

Huku mama Umazi Mwaruwa Makutu ambaye hapo awali alitoa mazao yake shambani kabla yakomae akikiri kufaidika pakubwa na sing’enge hiyo ya Kasaine.

‘Tulipokuwa hatujapata hii sing’enge tulikuwa tunatoka mkono mtupu kila msimu, hii sing’enge inasaidia mara mbili ,kwanza ukisikia kibati kinalia utajua tu kuna ndovu karibu, pili ndovu wenyewe kuingia ni vigumu mpaka wasukume mti ndio waweze kuingia shambani, na kitambo wafanye hivyo mkulima atakuwa amesikia na atatoka nje kumfukuza kabla aharibu mimea’, alisema Umazi.

Shamba limezungushwa Singe'nge ya Kasaine

Peter Musyoki kutoka kijiji cha Ngambenyi alisema singe’nge hiyo ya Kasaine imekua msaada kwake kwani inampa taarifa mapema kabla ya hatari ya kuvamiwa na ndovu kutokea. Zaidi alisema inazuia ndovu hasa wageni kutoingia shambani mwake.

Kivuva Kimeli kutoka kijiji hicho cha Ngambenyi anayemiliki ekari 8 za shamba, alisema shamba lake limekuwa njia ya ndovu kwa miaka mingi.Hali iliyopelekea yeye kukumbatia singe’nge hiyo mara moja licha ya changamoto ya miti ya kuzungushia singe’nge hiyo kuliwa na mchwa na kuanguka.

Kutokana na hali hiyo basi, aliamua kuanza kupanda miti ambayo inasaidia kuzuia singe’nge hiyo na kwa wakati huo huo kulinda mazingira kwa kuongeza upanzi wa miti.

Thomas Mundia naye alisema hadi kufikia sasa anasubiri fidia kutoka kwa shirika la wanyamapori la KWS baada ya ndovu kuharibu ekari 2 za mmea wake wa mbaazi mwaka wa 2019.

Lakini kwa sasa anaonyesha matumaini ya kuwa mimea yake itakuwa salama, kwani singe’nge hiyo ambayo aliweka mwanzoni mwa mwaka huu imemsaidia.

‘Kuna karatasi tayari nilijaza ziko Voi na kwasasa nasubiri kufidiwa mimea yangu’, alisema Mundia.

 

Simon Kasaine alisema mbali na changamoto ya miti ya kuzuilia singe’nge hiyo kuliwa na mchwa, Wanawashauri wakulima kupanda miti ili kuitumia kuweka singe’nge hiyo na kwa wakati huo huo kulinda mazingira.

Huku wakipania kutafuta mbinu za kuziba kabisa njia ambazo ndovu wamekuwa wakitumia kwa miaka mingi.

Na ili kufanikisha mbinu hiyo kwa asilimia 100, wameweka kamera kwenye miti inayoshikilia singe’nge hiyo ili kujua tabia za ndovu wanapojaribu kuvamia mashamba hayo.

Kasaine alisema singe’nge hiyo ni rahisi kwa wakulima kujitengezea kwani haihitaji rasilimali nyingi. Sawia na kwamba ni salama kwa wanyamapori na haiwezi kuwadhuru kivyovyote.

Kwa sasa wameweka singe’nge hiyo kwa wakulima wa vijiji 3 vinavyopakana na mbuga za wanyama katika kaunti hiyo ya Taita Taveta. Na wanalenga kuendeleza katika mashamba mengine.

 

Kulingana na takwimu za mwaka wa 2018 kutoka kwa Kamati ya Fidia ya Wanyamapori ya kaunti ya Taita Taveta , Eneo hilo lilikuwa na kesi zaidi ya 20 ya vifo vinavyotokana na wanyamapori, Majeruhi 235 na kesi 452 za uharibifu wa mazao unaosababishwa na wanyamapori.

Jacob Orahle ni msimamizi wa shirika la wanyamapori nchini KWS kaunti ya Kwale, alisema uharibifu wa mazingira na ukame umeongeza mizozo kati ya wanyamapori na binadamu.

Huku akitoa wito kwa jamii zinazoishi maeneo yanayopakana na mbunga za wanyamapori kulinda mazingira,kama njia mojawapo ya kupunguza wanyamapori kuhama makazi yao na kuingia katika makazi ya binadamu.

Elizabeth Gitari ni wakili wa maswala ya sheria kuhusu mazingira, alisema wakulima wana haki ya kuomba fidia pindi mazao yao yanapoharibiwa na wanyamapori.

 

Alisema tangu mwaka wa 2014 wakati sheria mpya ya wanyamapori ilipoanza kutumika, wakulima walikuwa bado hawajalipwa.

Lakini mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka wa 2021, serikali ilitoa zaidi ya shilingi milioni mia tano kwa ajili ya kuwalipa wakulima fidia kutoka mwaka huo wa 2014 hadi mwaka wa 2021.

Alitoa wito kwa wakulima hasa wanaoishi maeneo ambayo yamepakana na mbunga za wanyamapori kufanya kazi kwa ushirikiano na shirika la wanyamapori nchini kwa usalama wao na hata mazao yao.

‘Wakulima wanapaswa kuwa na uhusiano wa karibu na shirika la wanyamapori la KWS,na kuwaita KWS wakati wanyamapori wanatishia kuingia shambani mwao, nawashauri pia wakulima watumie singe’nge ambazo hazidhuru wanyamapori na pia ambazo zinalinda mazao yao’, Alisema Bi Gitari.

Wakulima wakiweka Singe'nge ya Kasaine

---