Zaidi ya wakulima 500 kutoka eneo la Tiwi huko Matuga kaunti ya Kwale wanakadiria hasara ya mimea shambani kuharibiwa kufutia mzozo wa umiliki wa ardhini ya Mbela katika eneo hilo.

Wakulima hao wakidai kuwa maafisa wa usalama ndio walitekeleza uharibufu huo.

Wakulima hao wakiongozwa na Mohammed Mwinyi, wanadai kuwa maafisa hao waliharibu mahindi pamoja na mimea Mingine waliyokuwa wamepanda katika ardhi hiyo ya ekari elfu moja inayozozaniwa baina ya wakaazi na bwenyenye mmoja.

Kulingana na wakaazi hao, wamekuwa wakiishi eneo hilo kwa muda wa miaka 30 wamedai kuwa mahakama iliwapa agizo la kulima katika ardhi hiyo inayodaiwa kukodishiwa bwenyenye huyo baada ya muda wa kukodi kutamatika mwaka wa 2013.

Kwa upande wake afisa wa shirika la kijamii la African Centre For Corrective and Prevention Action (ACCPA) Rashid Bagu ameshtumu vikali hatua ya maafisa hao kwa kuwahangaisha wakulima.

Hata hivyo Bagu ameahidi kuwa shirika hilo linalenga kuanzisha mchakato wa kutafuta haki ya wakaazi ya kumiliki ardhi hiyo katika bunge la kitaifa.