Huku ulimwengu ukiadhimisha wiki ya kunyonyesha,waraibu wa dawa za kulevya kanda ya Pwani wametakiwa kuwanyonyesha watoto wao ili wapate afya bora.

Wito huo umetolewa na daktari Daniel Wanyama kutoka kituo cha kurekebisha tabia waraibu wa dawa za kulevya cha ReachOut Centre Trust kilichoko jijini Mombasa.

Daktari Daniel ametaja kuwa watoto wanaonyonya maziwa ya mama zao ambao ni waraibu ama wale walio katika harakati za kujinasua hawawezi dhuriwa na maziwa hayo.

Ametaja kuwa maziwa hayo yanasaidia kupunguza chembe chembe za mihadharati ambazo zingemuathiri mtoto.


Kauli ya dkt.Daniel imetiliwa mkazo na Pauline Mtinda ambaye aliwahi kuwa mraibu wa dawa za kulevya na pia ni muathiriwa wa virusi vya Ukimwi.Pauline anasema alifuata ushauri wa wahudumu wa afya na kumyonyesha mtoto wake punde alipojifungua na sasa yuko na afya njema.

Wakati huo huo dkt.Daniel amewasihi waraibu hao kufuata maagizo wanayopewa na wahudumu wa afya,kutembelea vituo vya afya wanapokuwa wajawazito na hata baada ya kujifungua,sawia na kukoma kuwatoroka watoto wao pindi wanapojifungua.