Baada ya matokeo ya kura za mchujo katika chama cha ODM za wadhfa wa wawakilishi wadi kaunti ya Mombasa kutangazwa hapo jana, sasa wapinzani walioshindwa kwa wazi wameombwa kushirikiana na washindi kwa manufaa ya wakaazi.

Akizungumza na mwanahabari wetu mwaniaji wa kiti cha wadi ya Mji wa Kale Abdirahman Hussein ambaye alitangazwa na bodi ya kitaifa ya uchaguzi ya chama cha ODM kuwa mshindi na ambaye atapeperusha tiketi ya ODM katika uchaguzi mkuu ujao, amesema kwamba kura hizo za mchujo hazifai kuwatenganisha washindani hao bali yafaa waungane na kushirikiana namna watakavyoshinda uchaguzi mkuu ujao na kumhudumia mkaazi wa Mji wa Kale.

Abdirahman ambaye alikuwa akishindana na wenzake watano kunyakua tiketi ya ODM alipata kura zaidi ya 500 akifuatwa na Salim Rashid, mwakilishi wa sasa wa wadi hiyo Murfad Hashim Amur, Saddam Ahmed, Mohamed Hatimy na kisha Al-Amin Alwy Amin.

Aidha, Mwaniaji huyo amewashukuru wakaazi wa Mji wa Kale waliojitokeza na kumuwezesha kuishinda tiketi hiyo.

Katika matokeo hayo Priscila Mumba alitangazwa kuipeperusha tiketi ya ODM wadi ya Shimanzi Ganjini, Fatma Kushe- Kadzandani, Fadhili Makarani- Portreiz, Shariff Omar- Tononoka, Amriya Juma Boi- Mjambere, Shika Adabu- Juma Mwalimu miongoni mwa matokeo hayo.

Aidha baadhi ya matokeo ya baadhi ya wadi kama vile Magogoni na Mtopanga yalifutiliwa mbali kutokana na zoezi la uchaguzi kukumbwa na sintofahamu, huku baadhi ya wapinzani wakipinga matokeo ya baadhi ya maeneo.

 Mwandishi- Ibrahim Juma Mudibo