Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Sebastien Desabre amesema anatumai timu yake itatumia mechi hii ya nusu-fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON ili "kuwafariji" raia wa Kongo.

Sebastien Desabre amesema anatarajia kuwa timu itawapa burudani la soka wakongo wanaoteseka kutokana na ghasia zinazoendelea mashariki mwa taifa hilo.

Desabre amewaambia waandishi wa habari mjini Abidjan kwamba mechi ya leo dhidi ya wenyeji Ivory Coast ni maalum, na wanataka watu wanaoteseka huko Kongo wajivunie timu yao ya taifa na kwamba ni kazi yao kuwapa watu furaha na kuwafanya watabasamu.

DRC itatumia ngarambe hiyo ya Nusu fainali kutuma ujumbe na kutoa pole kwa waathiriwa wa mapigano Kaskazini mwa nchi hiyo.

DRC Wamesema kuwa hawatavaa jezi kwa ajili ya kupata ushindi bali kutuma ujumbe lakini pia na kutoa pole kwa wahanga wa mapigano lakini pia na kuomba maridhiano kati ya Serikali na Waasi.

Nahodha wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Chancel Mbemba amechapisha ujumbe unaosema kuwa “Naomba mara kwa mara nchi yangu iweze kurejea katika hali ya utulivu na watu wapate amani”.

Kocha wa DRC ambaye ni raia wa Ufaransa amefanya mabadiliko makubwa katika timu hiyo tangu alipochukua mikoba mwezi Agosti mwaka 2022 baada ya Kongo kupoteza mechi zao mbili za mwanzo za kuwania kufuzu kwenye michuano hiyo.

Katika mechi za leo Jumatano (07.02.2024) za nusu fainali ya michuano ya AFCON, timu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itachuana na Ivory Coast huku Nigeria ikishuka dimbani na Afrika Kusini.

Nigeria ambayo mchezaji wake nyota Victor Osimhen atakuwa uwanjani leo baada ya kuwepo hofu kwamba huenda angeukosa mchezo huo muhimu kutokana na jeraha.

Licha ya wachambuzi wengi wa soka kusema kuwa Nigeria na wenyeji Ivory Coast wana nafasi kubwa ya kushinda mechi za leo, dakika 90 ndizo zitakazoamua timu gani zitakazotoana kijasho kwenye fainali ya AFCON.

 


 

More Stories

Miraa na Mgoka kupigwa marufuku Mombasa

Wanafunzi kurudi shuleni juma lijalo

Vita dhidi ya mihadarati vyapamba moto Pwani