Uchumi wa Kenya Umetajwa kuimarika kwa kasi ndogo kutokana na vizingiti mbalimbali huku nafasi za ajira zikifikia 816,600 mwaka jana.

Sekta ya kilimo, ambayo mara nyingi ilitajwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi ilichangia kushuka kwa sekta nyingine.

Kulingana na halmashauri ya takwimu nchini Kenya (KNBS) Idadi ya ajira mpya zilizoundwa mwaka jana zimepungua kwa 108,300 ikilinganishwa na mwaka uliopita wa 2021.

Pato la taifa lilikua kwa asilimia 4.8 na kufikia Shilingi trilioni 13.368 mwaka 2022, chini ya ukuaji wa asilimia 7.6 mwaka 2021.

Kulingana na utafiti wa kiuchumi wa 2023 ukuaji wa mwaka jana ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na huduma na sekta nyinginezo kama vile ujenzi na viwanda.

Ajira katika sekta ya kisasa na mfumo wa zamani ilipanda kutoka milioni 18.3 mwaka 2021 hadi milioni 19.1 mwaka 2022 huku ajira katika sekta ya kisasa ikirekodi ukuaji wa asilimia 3.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 5.9 mwaka 2021.

Nayo ajira katika sekta ya mfumo wa zamani ilikua kwa nafasi 702,900 hadi kufikia milioni 15.9, huku shirika la takwimu nchini KNBS ikibainisha kuwa sekta hiyo ilijumuisha asilimia 86.1 ya nafasi zote mpya za kazi zilizoundwa.