Kocha wa Goodhope fc inayoshiriki ligi ya primia ya Mombasa, Shem Lumumba amesema wachezaji wake zaidi ya kumi waliosaidia pakubwa kunyakua ubingwa wa ligi hiyo msimu uliopita waliondoka klabuni hapo baada ya kusajiliwa na klabu mbalimbali.

Shem ameongeza kuwa wamefanya sajili saba msimu huu huku pia wakikuza vipaji kwa kuchagua wachezaji wachanga waliopo klabuni hapo.

Aidha ameeleza kuwa changamato nyengine wanazokabiliana nazo ni kwamba baadhi ya wachezaji wake ni wanafunzi hivyo basi mara nyengine huwa vigumu kuwapata wachezaji hao.

Licha ya kutoanza msimu vizuri kocha huyo amesema bado ni mapema na ana matumaini ya kupanda kileleni mwa ligi hiyo huku wakiratibiwa kumenyana na Mantubila katika uwanja wa shule ya msingi ya Khadija saa tisa alasiri siku ya jumapili kwenye mechi kali ya dabi ya Kisauni.

Shem vilevile ametoa wito kwa mashabiki na jamii kujitokeza kwa wingi viwanjani kushabikia vijana wao wa nyumbani.

Amesema hatua ya jamii na mashabiki kushabikia wachezaji inawapa morali vijana kuendeleza talanta zao.

Amewataka wadhamini kujitokeza na kudhamini timu nyingi za hapa Mombasa zinazokosa udhamini hivyo basi kupelekea vipaji vingi kufifia.
Goodhope iko katika nafasi ya 9 na alama 10 kwenye msimamo wa ligi ya primia hapa Mombasa chini ya Mombasa county football association.

Taasisi ya fedha ya HFC imetia saini mkataba na shirikisho la riadha nchini AK utakaowezesha wanariadha wa humu nchini kupata nyumba kwa bei nafuu.
Kupitia ushirikiano huo, taasisi hiyo itawawezesha wanariadha pamoja na maafisa wengine wa shirikisho hilo nchini kununua nyumba kwa bei sawa na ile mipangilio ya shirika la utoaji wa mikopo ya nyumba yaani Kenya Mortgage Refinancing Company KMRC.
Vile vile wanachama wa shirikisho hilo watapokea mafunzo ya usimamizi wa fedha huku wakipata nafasi ya kufahamishwa umuhimu wa kujipanga na kumiliki nyumba katika uhai wao.
Afisa mkuu mtendaji wa taasisi hiyo ya HFC Robert Kibaara amedokeza kuwa wanalenga kupanua ushirikiano wao utakaowezesha uboreshaji wa maisha ya wanamichezo wa humu nchini kumiliki nyumba.
Ameongeza kuwa wakenya wengi wanategemea uwezeshaji wa kifedha ili kununua nyumba, na kama benki watajitahidi kuhakikisha ndoto za wakenya katika safari yao ya kumiliki nyumba inatimia.
Rais wa shirikisho la wanariadha nchini meja mstaafu Jack Tuwei amepongeza ushirikiano huo akisema maslahi ya wanariadha yataangaliwa nyema haswa wanapostaafu.
Tuwei amesema mara nyingi kumekuwepo na taswira ya wanariadha wa humu nchini kuishi katika maisha ya uchochole baada ya kustaafu licha ya kuiletea sifa nchini hii.
Ametoa wito kwa wanariadha kujiunga na mpango huo ili kuwekeza kwa kumiliki myumba za bei nafuu.
Mpango huo utawaunganisha wanariadha na waajenzi wa nyumba hizo kama inavyopendekezwa na serikali kupitia idara ya ujenzi na mipangilio ya miji.

 

Msimamizi wa timu ya Kadzandani inayoshriki ligi ya primia hapa Mombasa, Lucy Abuna anahofia kwamba huenda timu yake isishiriki kwenye mechi zao zilizosalia katika ligi hiyo ya primia kutokana na changamoto za kifedha.

Akiongea na Radio Rahma Abuna amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kushindwa kulipa pesa ya refa kwa kukosa mdhamini.

Ameongeza kuwa imekua vigumu kwake kumudu timu hiyo licha ya wachezaji wake kujitahidi kushinda ligi ya daraja la kwanza na ligi ya daraja la pili kabla ya kupanda daraja na kutinga ligi ya primia ambayo wanacheza kwa sasa.

Kwa sasa anawaza kuhusu kuachana na soka na huenda pia timu yake ikatoka kwenye ligi hiyo ya Mombasa .

Lucy ameongeza mara nyengine wachezaji wake hulazimika kucheza bila kula na ata kutembea mguu ili kushiriki mechi za ugenini.

Ameeleza kuwa presha hupanda hususan inapofika siku ya mechi huku akiongeza kwamba licha ya juhudi za kufikia jamii na viongozi ili kupata usaidizi hazikufua dafu, ameendelea kutoa wito kwa jamii na viongozi kusaidia timu hiyo.Kwenye mechi yao ya wikendi Kadzandani waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji wao Wanderers na wikendi hii ya tarehe 27 Mei wameratibiwa kupepetana na Daytona saa tisa unusu .

Kadzandani inavuta mkia kwenye msimamo wa ligi ya primia Mombasa ikiwa na alama tatu baada ya kupiga mechi saba.

Ligi hiyo ya Mombasa ina timu 16.

 

Show more post