MKONDO wa 13 wa mashindano ya mchezo wa golf yanayoendelea Safaricom Golf Tour yatafanyika katika uga wa Vet Lab Sports Club wikendi hii huku chipukizi zaidi ya 350 na wachezaji wa kulipwa wakitarajiwa kushiriki kwenye mashindano hayo.

Mashindano hayo yanajiri wiki moja baada ya Lieutenant Colonel Michael Mulwa kushinda mashindano ya mkondo wa 12 yaliyofanyika Kenya Airforce Base huko Eastleigh.

Mashindano ya wikendi iliyopita yalijumuisha mpango wa uhamasishaji unaofahamika kama “Golf Mataani” ambapo chipukizi kutoka eneo la Mathare walipata nafasi ya kujifunza mengi kuhusu mchezo huo wa golf.

Mashindano ya wikendi hii yatashuhudia wachezaji wa kulipwa wakimenyana jumamosi huku chipukizi wakiratibiwa kumenyana pamoja na mafunzo ya golf jumapili .

Madhumuni ya mafunzo ya golf ni kuwatambua wachezaji golf wanaochipuka .

Tangu kuanzishwa kwa Safaricom Golf Tour mwezi Januari, mashindano hayo yamevutia zaidi ya washiriki 7,000 walioshiriki kwenye mashindano mbalimbali, mafunzo ya golf kwa chipukizi na mpango wa uhamasisho.

Baada ya mashindano yatakayogaragazwa Vet Lab, ziara hiyo ya safaricom itaelekea Royal Golf Club tarehe 30th na 31st July kwa awamu ya mwisho na kuhitimisha na fainali kuu iliyoratibiwa kupigwa Agosti 6 huko Vipingo, Kaunti ya Kilifi.

Kama sehemu ya kukuza talanta za chipukizi, Safaricom imeshirikiana na wakfu wa chipukizi wa mchezo wa golf maarufu kama Junior Golf Foundation (JGF) kukuza talata za wachezaji wanaochipukia .

 

Show more post