Huenda Kadzandani ikajitoa kwenye ligi ya primia Mombasa
Msimamizi wa timu ya Kadzandani inayoshriki ligi ya primia hapa Mombasa, Lucy Abuna anahofia kwamba huenda timu yake isishiriki kwenye mechi zao zilizosalia katika ligi hiyo ya primia kutokana na changamoto za kifedha.
Akiongea na Radio Rahma Abuna amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo kushindwa kulipa pesa ya refa kwa kukosa mdhamini.
Ameongeza kuwa imekua vigumu kwake kumudu timu hiyo licha ya wachezaji wake kujitahidi kushinda ligi ya daraja la kwanza na ligi ya daraja la pili kabla ya kupanda daraja na kutinga ligi ya primia ambayo wanacheza kwa sasa.
Kwa sasa anawaza kuhusu kuachana na soka na huenda pia timu yake ikatoka kwenye ligi hiyo ya Mombasa .
Lucy ameongeza mara nyengine wachezaji wake hulazimika kucheza bila kula na ata kutembea mguu ili kushiriki mechi za ugenini.
Ameeleza kuwa presha hupanda hususan inapofika siku ya mechi huku akiongeza kwamba licha ya juhudi za kufikia jamii na viongozi ili kupata usaidizi hazikufua dafu, ameendelea kutoa wito kwa jamii na viongozi kusaidia timu hiyo.Kwenye mechi yao ya wikendi Kadzandani waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya wenyeji wao Wanderers na wikendi hii ya tarehe 27 Mei wameratibiwa kupepetana na Daytona saa tisa unusu .
Kadzandani inavuta mkia kwenye msimamo wa ligi ya primia Mombasa ikiwa na alama tatu baada ya kupiga mechi saba.
Ligi hiyo ya Mombasa ina timu 16.