Kamati Kuu ya chama cha Orange Democratic Movement (ODM) imependekeza gavana wa kaunti ya Mombasa kuwa mmoja wa manaibu viongozi wa chama hicho.

Gavana Abdulswamad Shariff Nassir amependekezwa kuchukua wadhifa huo ulioachwa na waziri wa madini na uchumi samawati Hassan Ali Joho na yule wa vyama vya ushirika na biashara ndogondogo Wycliffe Oparanya.

Kupitia taarifa, Nassir amesema kipaumbele chake kitakuwa kuhakikisha kinara wa chama hicho Raila Odinga anashinda uwenyekiti wa AU, kuunganisha wanachama, kupigania uongozi bora, haki na sheria na vile vile kulinda ugatuzi.

Wengine wawili waliopendekezwa katika wadhifa wa naibu kiongozi wa chama ni gavana wa Kisii Simba Arati na seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga amependekezwa kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho.

Mabadiliko hayo yamefanywa katika mkutano ulioongozwa na kinara wa chama Raila Odinga.