Viongozi wa dini ya kiislamu wametoa wito kwa wanandoa watarajiwa kujiunga na kozi ya mafunzo ya ndoa kabla ya kuoana.
Viongozi hao wamesema mafunzo hayo yatasaidia jinsi ya kuishi na mwenziwe ndani ya ndoa.
Akizungumza katika hafla ya kuzindua kozi ya kuwafundisha wanandoa watarajiwa iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Quba, Sheikh Abdulaziz Muhammad amesema kuwa kunafaa kuwa na mikakati ya kutowaozesha wale ambao hawajapewa mafunzo hayo.
Kwa upande wake Sheikh Abu Hamza ametaja sababu ya kuvunjika kwa ndoa nyingi ni kufeli kwa malezi ya wazazi katika familia zao akitaka wazazi wawajibikie watoto wao ili kujenga tabia nzuri ya vijana.
Wakili Khadija Yusuf amesema kuwa kozi hii itahamasisha kizazi kijacho jinsi ya kuishi katika ndoa.
Ndoa ni nguzo muhimu katika dini ya kiislamu na kozi hii inalenga kuwafafanulia vijana maana haswa ya ndoa, faida ya ndoa, changamoto zake na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo ili kupunguza idadi kubwa ya kesi za talaka zinazoshuhudiwa.