Maafisa wa usalama eneo bunge la Kinango kaunti ya Kwale wanachunguza kisa ambapo watu 3 wa familia moja wamefariki huku mmoja akiachwa hali mahututi katika kijiji cha Malandi huko Kinango usiku wa kuamkia leo.

Watatu hao ni baba na wanawe wawili kati ya umri wa miaka 5 hadi 10 anaodaiwa kuwaekea sumu ambayo haijafahamika kwa sasa.

Kulingana na mkuu wa polisi eneo hilo Fredrick Ombaka, marehemu Ali Mwazuma Rashid mwenye umri wa miaka 36 anadaiwa kutekeleza unyama huo kabla ya kujitia kitanzi na kuokolewa japo kufariki akipokea matibabu katika hospitali ya Kinango.

Hata hivyo marehemu anadaiwa kusongwa na mzozo kati yake na wakweze  kulingana na ujumbe aliouandika kabla ya kujitoa uhai.

Leila Mwazuma aliye katika hali mahututi anaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya Kinango huku miili ya 3 hao ikilazwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali hio ikisubiri upasuaji.